Step by Step yazidi kupamba moto Kibaha Vijijini


25, April 2024.


Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Pwani Ndg. David Mramba ameendelea kuwasha moto kwa kutoa  Mafunzo katika Kata za Kwala, Dutumi, Ruvu na Kikongo zilizoko Tarafa ya Ruvu Wilaya ya Kibaha Vijijini.

Katika Mafunzo hayo ambayo washiriki walikuwa na shauku kubwa ndg. Mramba amesema Kiongozi ni mwanachama yeyote wa CCM aliyepewa dhamana ya Uongozi na Taasisi au Wananchi kwa kuchaguliwa au kuteuliwa ambaye ana wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa dhamira ya kweli.

Amesema kuongoza ni kuonyesha njia, ni kuwafanya unaowaongoza waone fahari kukuona uko mbele yao na wao wanakufuata, wanakufuata sio kwa sababu wanakuogopa, bali kwa sababu wanakuamini na Imani ya kweli hupatikana kwa vitendo vyako.

Ndg. Mramba ameendelea kusema kuwa Viongozi sahihi wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, kuaminiana, kusaidiana, kusikilizana, kuelewana na kushauriana ili waweze kufikia lengo la kuwa Viongozi kama walivyoaminiwa na Wanachama wenzao.

Pia, amesema Wanachama walipowachagua Viongozi hao walitambua Chama kitakuwa mikono salama na wataongoza vizuri na kusababisha Wananchi kuikimbilia CCM kwa utashi wao.

Aidha, amesema katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji Viongozi hao wanapaswa kufanya utafiti wa kina ili kuwapata Wagombea wanaokubalika katika jamii, waadilifu na wasiotiliwa Mashaka hata kwenye sifa za Kisheria.

Viongozi hao wa Kata na Matawi wametakiwa kutenda haki kwenye vikao vya uteuzi bila kuweka upendeleo kwa ndugu zao, rafiki zao na wengineo ili kuleta uwiano katika kuwapata Wagombea bora na si bora Wagombea.

Pamoja na Mafunzo hayo Ndg. Mramba ameweza kuwatembelea Waathirika wa Mafuriko wa kaya zisizopungua 30 Katika Kata ya Kwala, Kijiji cha Kwala ambao nyumba zao zimeharibiwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hadi kupelekea wananchi hao kwenda kuishi kwenye nyumba za Majirani na ndugu zao wa karibu.

Ndg. Mramba ameshirikiana na Wananchi walioathirika na mafuriko kwenye  zoezi la kuchimba mtalo wa kupitisha maji kutoka kwenye makazi ya watu na kuyaelekeza mashambani.

Mwisho, amewataka Waathirika hao kuwa wavumilivu kwani Serikali inayoongozwa na Mhe, Daktari Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sikivu na inatekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuwajali wananchi wake.


*STEP BY STEP*

*2024 PWANI YA KIJANI*


*Tukutane site*


Taarifa hii imeandaliwa na:

Idara ya Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM,

Mkoa wa Pwani.

No comments