Waganga wa kienyeji, manabii wa makanisa, wote ni wapigaji

 


Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, imeiga utamaduni kutoka nje, baada ya ule wa kwake kubezwa na kuonekana wa kizamani. Zamani tunazoambiwa, hakukuwa na Ukristo wala Uislamu katika Afrika, bali jamii ziliabudu kwa mujibu wa tamaduni zao. Wapo waliofanya ibada zao chini ya miti, wengine mtoni, wengine njia panda, bondeni, ,mashambani na hata kwenye miamba.

Ujio wa dini hizi za kisasa, ulizifanya imani hizi za zamani kutoweka kutokana na kizazi kubadilika. Wageni waliwapeleka watoto shuleni na kuwafundisha utamaduni wa dini mpya, taratibu vizazi vikaanza kubadilika na hadi hivi  sasa, ni nadra kukuta jamii ikiabudu katika mapango, miti, mtoni au mashambani.

Ukiona hivyo katika nyakati hizi za sasa, kinachofanyika ni tambiko la jamii au koo. Kwa mfano, wapo  ambao huenda kufanya matambiko kwa ajili ya kuwakumbuka wafu wao, au kuomba ili kupatiwa vitu fulani kwa njia za kiasili. Matambiko haya, yanayofanyika kote barani Afrika, ni tofauti na imani za kishirikina.


Imani za kishirikina kwa jamii za Kiafrika ni jambo la jadi. Miaka na miaka, watu wa bara hili wamekuwa wakiabudu uchawi. Uchawi katika baadhi ya sehemu, husaidia kuzuia au kuleta mvua, jua, mafuriko, kimbunga na mabalaa mengine ya kiasili.

Uchawi pia inasemekana katika baadhi ya sehemu, husaidia watu kupata ajira, utajiri, umaarufu, sifa na wakati mwingine huweza kuwadhuru watu kwa namna mbalimbali. Zaidi ya asilimia sabini ya waafrika ni waumini wa imani za kishirikina.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la makanisa yanayojigawa kutoka makanisa makubwa yaliyoletwa na wazungu. Makanisa hayo sasa yamegeuka kuwa mali binafsi za waanzilishi wake na ndiyo maana ni rahisi kusikia kanisa likitajwa kwa jina la mtu.

Ni makanisa machache ambayo yameweza kuwekeza angalau nusu ya mikoa yote nchini, lakini mengi yao yapo eneo moja, yakishamiri zaidi jijini Dar es Salaam. Kila mtaa una kanisa na mchungaji wake. Kazi yao ya kulitangaza neno la Mungu hufanya hadi usiku wa manane na mengi kati yao, yana miujiza.

Ni kawaida siku hizi, kwenye haya makanisa, kuambiwa mtu huyu alikuwa na mapepo wabaya, lakini sasa ameondolewa. Tuna mashuhuda wengi wanaoelezea kadhia mbalimbali walizopitia kabla ya kusaidiwa na Mchungaji, Nabii, Pastor na kadhalika. Miujiza hii, haikuwahi kuripotiwa kwa miaka mingi na Kanisa Katoliki, Anglikana au hata Pentekoste!


Taratibu ukweli wa makanisa haya unaanza kujionyesha. Ni matapeli. Mchungaji maarufu barani Afrika, TB Joshua, ambaye sasa ni marehemu, imethibitika kwamba katika mafundisho na mahubiri yake yaliyojaa maajabu, kumbe alikuwa ni mwongo, aliyewapanga watu wa ushuhuda wa uongo ambao wameifanya kazi hiyo kwa miaka zaidi ya 20.

Si yeye tu, kwani kabla ya hapo, wapo manabii na wachungaji katika Afrika waliwahi kuumbuka. Kusema kuorodhesha orodha yao hapa, inaweza kujaza kurasa hizi bila kufikisha ujumbe unaokusudiwa.

Jambo la msingi na ukweli ni kwamba manabii hawa wa makanisa, hawana tofauti na waganga wa kienyeji. Kama kweli wachungaji hawa wanaofanya miujiza wana uwezo wa kuwaponya watu wenye magonjwa yaliyoshindikana, mbona hawaendi mahospitalini kuwanyenyua watu waliolala kwa kuzidiwa na magonjwa kama Kansa, Moyo, Figo na mapafu?

Watanzania na waafrika kwa ujumla wao, wanaibiwa wakijiona kutokana na ujinga wao wenyewe. Wa kutaka mambo mepesi, kwa haraka. Mganga wa kienyeji anakudanganyaje na wewe ukakubali kwamba anaweza kukupa utajiri wakati yeye mwenyewe, ili akufanyia ndumba hizo anataka umpe hela?

Kwa nini asijipe mwenyewe mamilioni hayo akaishi kwa starehe badala ya kukimbizana na wewe? Uganga na Uchawi upo, lakini si kwa utajiri, bali kwa kusaidia machukizo madogomadogo ya kimazingaombwe.

Ukitaka kujua utapeli wa manabii wetu, angalia shuhuda zinazotolewa. Eti mtu katapika kiwembe! Hivi mtu anatapikaje wembe kweli? Mtu kajisaidia mijusi, katapika hirizi!! Yaani wao wanataka kutuaminisha kuwa maisha yetu yametawaliwa na uchawi.

Ni lazima watupeleke kwa uchawi kwa sababu na wenyewe wanaabudu uchawi. Mifano ipo mingi inayoonyesha kuwa manabii hawa huwapanga wagonjwa wanaoonekana katika luninga wakitudanganya kuwa walikuwa hivi na vile.

Si lengo langu kukuambia uachane na imani yako kwa nabii unayemuamini, lakini nataka kabla hujachukua senti yako kuipeleka kanisani ili kutoa sadaka, jiongeze. Umewahi kuwaona matajiri wakubwa unaowajua wakitolewa mapepo? Mbona masikini tu ndiyo hutolewa mapepo, tena kwa gharama? 

SHTUKA!

No comments