Muundo wa jengo linalofanana na pedi wazua gumzo mitandao

 

Muundo unaopendekezwa wa kituo cha treni katika mji wa Nanjing nchini China umevutia watumiaji wa mtandao wa China - kwa sababu zote zisizo sahihi.

Mamlaka zinasema muundo wa kituo cha Nanjing Kaskazini ulipata msukumo kutoka kwa maua ya plum, ambayo ni maarufu katika jiji hilo.

Lakini mtandaoni, wengine wanaashiria kufanana kwake na kitu tofauti – pedi au sodo za wanawake wanazovaa wakiwa kwenye hedhi.

"Hii ni pedi kubwa. Inatia aibu kusema kuwa inaonekana kama maua ya plum," mmoja alisema kwenye tovuti ya kijamii ya Weibo.

Mada hiyo imesababisha gumzo kwa mamilioni ya watu katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii ya China.

"Kwa nini sote tunaweza kusema kuwa ni pedi mara moja, lakini wasanifu hawawezi?" mtumiaji mmoja wa Weibo alisema.

"Nadhani tunapaswa kuchukua nafasi hii kuitaka jamii kuzingatia unyanyasaji dhidi ya hedhi. Ubunifu huu uko mbele ya wakati wake," mtumiaji mwingine alitania.

Kulingana na gazeti linalomilikiwa na serikali la Nanjing Daily, muundo wa awali uliangaziwa na serikali ya jimbo la Jiangsu na Kampuni ya Reli ya Jimbo la China.

Ujenzi unatarajiwa kuanza katika nusu ya kwanza ya 2024, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

BBC

No comments