Jihadhari, Kukopa au kukopesha ni hatari!

 

PENGINE kichwa cha habari cha makala hii, kinaweza kukupa maswali mengi, lakini huo ndiyo ukweli katika dunia ya sasa. Wakati fulani nikifanya kazi katika taasisi moja binafsi, tulikuwa katika mkutano wa kawaida kati yetu waajiriwa na mwajiri, kijana mwenzetu wa Kitanzania ambaye alibarikiwa.

Alikuwa na kawaida ya kututia moyo, kwamba tukitaka kufanikiwa katika maisha, lazima tufanye kazi kwa bidii, lakini tukilenga kujiajiri. Hatuwezi kutajirikia katika kazi yake, kitu ambacho tulimshangaa sana kwani si waajiri wengi huwafumbua macho watu waliowaajiri.

Katika mazungumzo hayo hata hivyo, alitueleza kuwa na katika kuutafuta utajiri, kamwe hatuwezi kuupata bila kupata mikopo. Iwe kutoka kwa watu binafsi au taasisi, kwa sababu katika kukua kibiashara, kunahitaji uwekezaji mkubwa.

Yes, watu wanakopa iwe katika taasisi kubwa za kimataifa, za kitaifa na hata taasisi ndogo ndogo zilizosajiliwa na watu binafsi, kila mmoja akiwa na vigezo vyake kulingana na eneo na kiwango cha hela. Watu binafsi, ambao mara nyingi huwa na masharti nafuu kuliko taasisi, wana riba kubwa.

Wanakuwa na riba kubwa kwa sababu ya risk kubwa waliyonayo katika kurejesha fedha zao kwa sababu kwanza wanafanya kinyume cha sheria, ni rahisi kurukwa. Maana hata kama mnaweza kuandikishana, lakini aliyekopesha atakapokwenda mahakamani, atashindwa kwa sababu sheria haimpi mamlaka ya kukopesha.

Hii inafanya mikataba ya kukopeshana inayoingiwa baina ya watu binafsi, mara nyingi inakuwa ni ya ujanja ujanja, ambayo inambana mkopaji kiasi kwamba ni bora alipe anachodaiwa kuliko kupelekana mahakamani.

Lakini kwa nini ninasema kukopa ni hatari na ni kifo? Hii inatokana na matukio ambayo nimeanza kusimuliwa kwa miaka mingi na ambayo baadhi ya simulizi hizo ninawajua wahusika. Na si tu kukopa, bali ni hatari kwako pia hata kukopesha.

Wakati flani enzi za kusoma shule za msingi, niliishi Singida. Kwa udogo wa mji ule, ilikuwa ni rahisi kuwafahamu wafanyabiashara, wahindi, waarabu na hata wazawa. Sasa baada ya miaka mingi ya kuhama kutoka kule na kujichanganya kwenye maeneo mengine, siku moja nikakutana na rafiki yangu wa enzi hizo.

Stori nyingi za Singida, mara unamkumbuka yule, huyu na flani? Katika kukumbushana, tukafika kwa mfanyabiashara mmoja ambaye alikuwa na tabia ya kutoa pipi kwa watoto, kila tukienda kununua chochote dukani kwake miaka hiyo, akasababisha watoto kuwa wengi dukani kwake. Jamaa akasema ‘walimuua bwana..’!

Ilikuaje? Jamaa alikua na kawaida ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo bidhaa kwa mali kauli, wao wanaenda kuuza minadani halafu mwisho wa wiki wanamlipa, wanachukua mzigo mpya. Sasa inadaiwa kuna jamaa walichukua mzigo mkubwa, kulipa wakaona tabu. Kwa hiyo ili kurahisisha, wakapanga njama, usiku wakamvamia na kumuua!

Kesi hizi ziko nyingi kutokana na simulizi. Lakini si kuua tu, wengine wanakopesha lakini hawana wema na wewe. Kuna watu wanakukopesha kwa mfano, unaweka dhamana labda kibanda chako (nyumba). Muda wa kulipa ukifika, mkopeshaji hapatikani kwa simu wala kazini au nyumbani kwake. Halafu baada ya wiki mbili au mwezi mbele, anaibuka na kudai hataki hela, ila kwa kuwa umekiuka mkataba, anataka nyumba.

Mtavutana lakini kwa kuwa hawa watu wana mitandao, wanashinda kesi na kujikuta umeuza nyumba yako yenye thamani ya milioni 50 kwa milioni tano tu labda. Na wengine, ingawa hili ni la kiimani zaidi, wanadai unakopeshwa, halafu muda wa kulipa ukikaribia, unarogwa, ama unasahau kulipa, au unapata upungufu wa afya ya akili!

Sasa hiyo ni kukopa. Hali iko hivyo pia kwa kukopesha. Unampa mtu, ambaye mara nyingi ni yule unayemuamini, kiasi kikubwa cha fedha ukiamini atarejesha, lakini bahati mbaya, ama mambo yanakwenda kombo au kwa sababu tu ya tamaa, anaona bora akuue ili awe huru!

Nimeandika hivi kwa sababu kuna habari imetokea siku mbili hizi zilizopita kule Afrika Kusini imeniuma sana. Kuna Mtanzania mmoja alikuwa na makazi yake nchini Msumbiji, akifanya shughuli zake. Wanasema ni mwenyeji wa Kinondoni Dar es Salaam.

Sasa kwa namna wanavyosema, alikuwa amemkopesha Mtanzania mwenzake mmoja ambaye yeye alikuwa anaishi Johannesburg, Afrika Kusini. Katika kudaiana, yule mdaiwa, akamwambia mdeni wake aende Sauzi, ili akampatie chake.

Kufika kule akawasiliana na mkewe aliyemuacha Msumbiji kuwa amefika salama, lakini baada ya hapo hakupatikana tena hadi siku tatu baadaye mwili wake ulipopatikana katika moja ya hospitali jijini humo, akiwa amepigwa risasi na watu wasiojulikana.

Ni ngumu kusema aliyemkopesha ndiye aliyemuua kwa sababu hakuna uthibitisho, lakini ni rahisi kupata dhambi ya kuunganisha doti na kuweze kumhisi.

Katika maisha haya ni vigumu kuishi bila mikopo, lakini ni kitu cha msingi sana kuwa makini na kiasi cha mikopo tunayokopa au kukopeshwa, maana wakati mwingine badala ya kutusaidia ili kupunguza ukali wa maisha, inatufanya kuwa ndicho chanzo cha kupoteza kabisa maisha.

Kama ni lazima, ni vyema kukopa kiwango kidogo cha fedha ambacho kwanza hautashindwa kukilipa hata kama ni kidogo kidogo, lakini pia hata mkopeshaji wako hawezi kutetereka kwa wewe kushindwa kulipa deni. Ingawa hata hivyo, kiwango kidogo cha deni unalodaiwa haiwezi kuwa sababu tosha ya kutopata madhara kwa kushindwa kulipa.

Ushahidi wa matukio ya watu kupigana visu na mapanga, hasa jijini Dar es Salaam kwa sababu ya kudaiana shilingi mia moja au mia mbili unathibitisha hili. Kitu cha msingi kabisa katika kukabiliana na madeni unayodaiwa, ni kuwa na lugha ya kunyenyekea kwa mdeni wako. Haipendezi, unadaiwa halafu unatoa lugha inayompa hasira mdeni wako kama vile..”nini bwana weee, hela yenyewe shin’ ngapi unanisumbua?”

Hizi ni lugha ya kupandishana presha. Yaani uje kwangu mikono nyuma uombe nikukopeshe elfu kumi, halafu kesho nikufuate unilipe unipe majibu kama haya, yanaleta hasira. Kwa hiyo lugha, hasa ya staha ni silaha ya kwanza kuitumia kwa mtu anayekudai. Unyenyekevu katika kulizungumzia deni lako linamfanya hata anayekudai aamini unachomwambia, hata kama yeye atapanda juu kwa hasira.

Kwa wale tulio na baraka za kuweza kuwakopesha wengine, siyo kila mkopaji ni mwema kwako, hata kama ni rafiki yako kipenzi, ndugu au jamaa unayemuamini. Imethibitika mara nyingi kwamba fedha ni shetani asiye na wema, kwani hata baadhi ya watoto hupanga njama za kuwaua wazazi wao ili warithi mali mapema!

Kopesha kwa kiasi, dai kwa staha. Kitu salama kabisa, ni kuepuka kukopesha. Kama umebarikiwa kuwa na ziada, ni bora kutoa misaada kuliko kukopesha kibinafsi. Vinginevyo, sajili taasisi, kwani deni la taasisi halifi.

Vivyo hivyo, ni bora kukopa kwenye taasisi zilizosajiliwa kuliko kwenda kwa mtu binafsi. Watu wa benki hawawezi kupanga njama za kukudhuru kwa sababu fedha ile haina mwenyewe, sana sana watakupeleka mahakamani ambako utashinikizwa kulipa kwa mujibu wa sheria.

 

No comments