Putin asema makubaliano yanaweza kufikiwa ili kumwachilia huru ripota wa Marekani

 

Rais Vladimir Putin amesema anaamini makubaliano yanaweza kufikiwa ili kumwachilia Evan Gershkovich, ripota wa Marekani aliyezuiliwa mwaka jana nchini Urusi.

Akizungumza na mwenyeji wa Marekani Tucker Carlson, Bw Putin alisema mazungumzo yanaendelea na Marekani kuhusu mwanahabari huyo ambaye anazuiliwa kwa tuhuma za ujasusi.

Katika mahojiano hayo, Bw Putin alizungumza kuhusu Ukraine, marais wa Marekani na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Urusi kuketi na mwandishi wa habari wa nchi za Magharibi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.

Bw Putin alisema anaamini makubaliano yanaweza kufikiwa ya kumwachilia Bw Gershkovich, 32, "ikiwa washirika wetu watachukua hatua za kuafikiana".

"Huduma maalum zinawasiliana. Zinazungumza... naamini makubaliano yanaweza kufikiwa."

Bw Gershkovich, ripota wa Wall Street Journal, alikamatwa katika jiji la Yekaterinburg, takriban kilomita 1,600 (maili 1,000) mashariki mwa Moscow, tarehe 29 Machi mwaka jana.

Mnamo Januari, Urusi iliongeza tena kizuizi chake cha kabla ya kesi hadi mwisho wa Machi. Anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela iwapo atapatikana na hatia.

Bw Carlson alimuuliza Bw Putin ikiwa atakuwa tayari kumwachilia ripota huyo mara moja na akasema: "Tutamrudisha Marekani."

Lakini rais wa Urusi alisisitiza kwamba Bw Gershkovich, ambaye bado hajahukumiwa, alikuwa amepokea taarifa za siri, na akadokeza ni nani Urusi ingekubali katika kubadilishana wafungwa.

Bw Putin alitaja "mtu, kutokana na hisia za kizalendo, [ambaye] alimuondoa jambazi katika mojawapo ya miji mikuu ya Ulaya... wakati wa matukio katika Caucasus".

Mahojiano hayo, yenye urefu wa zaidi ya saa mbili, yalirekodiwa huko Moscow siku ya Jumanne.

BBC


No comments