Biden awachekesha Wamisri baada ya kumwita Sisi 'rais wa Mexico'

 


Rais wa Marekani Joe Biden amewachekesha baadhi ya Wamisri baada ya kumtaja kimakosa Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi kama "rais wa Mexico".

"Kama unavyojua, mwanzoni rais wa Mexico, Sisi, hakutaka kufungua lango ili kuruhusu bidhaa za kibinadamu kuingia [Gaza]," Rais Biden alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa Alhamisi, wakati akitoa maoni juu ya vita vinavyoendelea kati ya Israel na Gaza.

Rais wa Mexico anaitwa Andrés Manuel López Obrador.

Baadhi ya Wamisri waliochanganyikiwa wametumia mitandao ya kijamii kueleza kuwa mkanganyiko huo ni wa ucheshi kwani kwa muda mrefu Wamisri wamempa jina la utani Rais al-Sisi "El Meksiki", ambalo tafsiri yake ni "The Mexican" ili kuepuka udhibiti.

"Huwezi kumkosoa rais kwa uhuru hivyo Wamisri wakaanza kumwita 'El Meksiki' ('Mmexican' kwa Kiarabu) kwa sababu inasikika kama 'al-Sisi' ili waepuke kuchunguzwa na kumkosoa kwa uhuru," mtumiaji mmoja alisema kwenye mtandao wa X (zamani ukijulikana kama Twitter).

"Inachekesha zaidi wakati nyote mnajua kwamba kweli nchini Misri tunamwita [Bw al-Sisi] 'El Meksiki' wa Mexico badala ya 'al-Sisi' ili asitambuliwe na serikali ya Misri," Mmisri mwingine aliweka ujumbe mtandaoni.

Nchini Marekani, mkanganyiko huo umezua wasiwasi kuhusu afya ya Rais Biden na uwezo wake wa kiakili, lakini kiongozi huyo amejitetea na kusema kuwa yuko sawa.

BBC

No comments