Watu wanne wafariki katika mapigano ya ubomoaji msikiti India

 

Takriban watu wanne wamefariki katika ghasia katika jimbo la kaskazini mwa India baada ya mamlaka kubomoa msikiti kwa madai kuwa ulijengwa kinyume cha sheria.

Ghasia zilizuka katika mji wa Uttarakhand wa Haldwani wakati wa kile polisi wanasema ni "hatua ya kupinga uvamizi".

Mamlaka imesema kuwa zoezi hilo lilizinduliwa ili kusafisha majengo haramu, ikiwa ni pamoja na msikiti na madrassa (shule ya kidini) inayopakana nayo.

Lakini Waislamu walioswali msikitini wanasema wamekuwa wakilengwa isivyo haki.

Mamia ya waandamanaji na maafisa wa polisi walijeruhiwa katika mapigano hayo yaliyozuka Alhamisi jioni.

Video zilionyesha waandamanaji wakichoma moto magari na kuyarushia mawe na polisi wakiwarushia mabomu ya machozi.

Amri ya kutotoka nje imewekwa na serikali imetoa maagizo ya "kupiga risasi mara moja" ili kudhibiti hali hiyo.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Banbhoolpura huko Haldwani.

Wilaya hiyo ilishuhudia maandamano makubwa Januari mwaka jana baada ya zaidi ya watu 50,000, wengi wao wakiwa Waislamu, kupewa notisi ya kufukuzwa kwa madai ya kuishi eneo hilo kinyume cha sheria katika ardhi inayomilikiwa na Shirika la Reli la India.

Ubomoaji huo baadaye ulizuiliwa na mahakama kuu ya India.

Maafisa walisema hatua ya hivi punde ilitokana na amri ya mahakama kuu inayotaka mamlaka kuondoa makazi haramu kutoka eneo hilo.

Wenyeji wamekanusha hilo na kusema kuwa msikiti huo ulibomolewa kabla ya mahakama kutoa uamuzi wa mwisho katika kesi hiyo.

"Wakati uongozi ulipokuja [kuvunja miundo] tuliwaomba wasimamishe hadi kikao kingine cha mahakama. Lakini hawakusikiliza. Kama wangesubiri uamuzi wa mwisho wa mahakama, kusingekuwa na upinzani [kutoka kwetu]. ," Shakeel Ahmad, diwani wa eneo hilo, aliliambia gazeti la Indian Express.

Mvutano kuhusu ubomoaji wa misikiti umeongezeka katika miezi michache iliyopita.

Makundi ya Kiislamu yanasema yanahisi kulengwa isivyo haki chini ya serikali ya Wahindu ya Waziri Mkuu Narendra Modi na kuishutumu kwa mgawanyiko wa kidini kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baada ya miezi miwili. Hata hivyo, serikali inakanusha madai hayo.


No comments