Jina kubwa haliakisi uhalisia wa mtu
Pichani..Kushoto ni Diego Maradona, Pele na Michel Platini
Picha hii ilipigwa mwaka 1986 wakati wa fainali za Kombe la Dunia, zilizofanyika nchini Mexico, ambako Maradona, akiwa nahodha wa Argentina alitwaa ubingwa huo.
FIFA, ambao wanasimamia soka duniani, walikua na kampeni kadhaa ambazo walitaka kuzitekelezakupitia soka, hivyo zikawateua watatu hao kuwa mabalozi wa kampeni hizo.
Kumbuka, Maradona akiwa na Napoli ya Italia, alikuwa hashikiki na alithibisha uwezo wake katika fainali. Na sidhani kama dunia inahotaji maelezo zaidi juu ya Platini, moja kati ya magwiji wa muda wote wa soka la dunia?
Pele, anayechukuliwa kuwa ndiye mwanasoka mahiri zaidi kuwahi kutokea duniani, ambaye kwa miaka yote akiwa hai alialikwa kwenye fainali zote, akiwa na rekodi ya kutwaa ubingwa wa dunia mara tatu akiwa na Brazil, alipewa nafasi ya kuwaongoza wadogo zake katika kampeni hizo.
Maradona alipewa ubalozi wa kupinga matumizi ya madawa ya kulevya katika soka, Platini akautwaa ubalozi wa kupinga rushwa michezoni na The GOAT Himself, Pele, akapewa heshima ya kuwa balozi wa kupinga unyanyasaji wa watoto duniani.
Unajua nini kilitokea?
Diego Maradona akiwa bado kinara wa soka la hadhi ya dunia, badala ya kupinga matumizi ya madawa ya kulevya michezoni, yeye mwenyewe ndiye akawa mwathirika mkubwa wa ubwiaji unga, kiasi kwamba aliondolewa katika orodha ya wanasoka wa Argentina wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Marekani mwaka 1994.
Michel Platini, baada ya kustaafu soka na kutaka uongozi ngazi ya Uefa, alifungiwa kujihusisha na mpira wa miguu baada ya kuthibitishwa kwamba alitumia rushwa aliyokabidhiwa kuipiga vita.
Lakini ishu kubwa zaidi ikaja kwa Pele. Mwamba huyo asiyepingika kwa ubora wa soka duniani, alitembea na dada wa kazi nyumbani kwake na kumpa mimba. Lakini baadae alimkataa mtoto aliyezaliwa, akisahau kwamba yeye ni balozi wa kutetea watoto.
Ilibidi binti huyo aliyepatikana kwa dada wa kazi aende mahakamani akidai Pele ni baba yake. Baada ya vipimo vya DNA, Mahalama nchini Brazil zikamtangaza Pele kuwa ni baba mzazi wa binti huyo.
Kwa masikitiko, binti huyo aliandika kitabu alichokiita BINTI ALIYEKATALIWA NA MFALME.
Nini tunajifunza?
Binadamu tuna tabia ya kudhani mwenye umaarufu, uwe wowote, kuna mambo hawezi fanya. Kuna tofauti kubwa kati ya umaarufu wa mtu na uhalisia wa hisia za kibinadamu!

Post a Comment