RAIS SAMIA AMTETEA FREEMAN MBOWE, AMJIBIA MASHAMBULIZI

Katika mitandao mingi ya kijamii, baadhi ya wadau wamekuwa wakitilia shaka uhusiano uliopo kati ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini (Chadema), Freeman Mbowe na Rais Samia Suluhu Hassan.

Viongozi hao wawili wamekuwa vinara wa mazungumzo yanayoendelea ya maridhiano ya kisiasa, baada ya miaka saba ya siasa za chuki, visasi na kuviziana.

Hata hivyo, pamoja na dhamira nzuri juu ya mikutano hiyo, kitendo cha Rais Samia kukubali kuhudhuria mkutano wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema, kumeongeza maneno mengi ya kejeli kwa wapinzani wa Mbowe.


Wengi wanaamini nyuma ya mikutano hiyo, yapo masilahi binafsi ambayo Mbowe kama mwanasiasa na kiongozi anayapata.

Kwamba amelambishwa asali kiasi sasa Chadema kimegeuka kuwa chama mshirika wa CCM badala ya kuwa mpinzani.

Hata hivyo Madam President Samia amemtetea Mwenyekiti huyo wa tatu wa Chadema, akisema hajapewa chochote zaidi ya kupigania ustawi wa taifa lake.

Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia katika mkutano huo wa Chadema, akiandika historia ya peke yake katika siasa za Tanzania.

No comments