BBC WAMTAZAMA RAIS SAMIA KIVINGINE BAADA YA KUHUDHURIA MKUTANO WA CHADEMA
Kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuhudhuria mkutano wa kisiasa ulioandaliwa na chama kikuu cha upinzani nchini kwake ni cha kihistoria si kwa taifa lake pekee bali karibu bara zima la Afrika.
Namna pekee ya kufahamu ukubwa wa tukio hili ni kulinganisha na nchi nyingine jirani au mbali na Tanzania. Fikiria, kwa mazingira ya sasa kama kuna uwezekano wa Rais William Ruto wa Kenya kualikwa kama mgeni rasmi kwenye tukio la chama kinachoongozwa na Raila Odinga.
Au Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuhudhuria tukio lililoandaliwa na chama cha upinzani cha NUP kinachoongozwa na Bobi Wine. Unaweza pia kusogea Zimbabwe na kutazama uhusiano baina ya Rais Emerson Mnangagwa na washindani wake akina Nelson Chamisa.
Hata kwa Tanzania, hii ni mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Uhusiano baina ya viongozi wa vyama vya upinzani na chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) haujawahi kuwa mbovu kupindukia ukilinganisha na nchi nyingine lakini bado tukio la leo kwenye mkutano ulioandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA) kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake ni la kipekee.
Jambo kubwa zaidi ni kwamba hili ni jambo ambalo lilikuwa mbali na mawazo ya Watanzania miaka miwili tu iliyopita. Katika historia ya zaidi ya miaka 60 ya Tanzania huru, hakukuwa na wakati kulipokuwa na uhusiano mbovu zaidi baina ya CCM na wapinzani kuliko miaka saba iliyopita.
Miaka mitano tu iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, alipigwa risasi 17 na kunusurika kufa katika tukio ambalo hadi sasa linahusishwa na siasa. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, viongozi wa ngazi za juu wa chama kikuu cha upinzani Zanzibar – ACT Wazalendo, walivamiwa na kupigwa na watu waliohusishwa na vyombo vya dola.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi nchini Tanzania, viongozi wa upinzani kama vile Godbless Lema, Lissu na Hezekiah Wenje, walikimbia nchi wakihofia maisha yao, sababu ikiwa ni siasa.
Katika miaka miwili ya utawala wake, waliokimbia nchi wamerejea na kwa ujumla hali ya kisiasa nchini Tanzania imeanza kurejea katika hali ilivyokuwa kabla ya utawala wa hayati Rais John Magufuli. Kwa vyovyote vile, hakuna alifikiri kwamba kuna siku Chadema au Bawacha wangeweza kumwalika Magufuli kwenye mkutano wao.
Lakini swali pekee ambalo wengi wanajiuliza na limetawala mijadala mitandaoni na midomoni mwa wengi ni kwamba, nini maana ya tukio hili la leo la Samia na pengine kwa nini anafanya anavyofanya?
Mwanamke mwenye moyo wa chuma
Imesadifu kwamba tukio la Samia kuhudhuria mkutano wa Chadema linaendana maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake. Na kama ambavyo siasa zisizo za kawaida na kutoyumba katika msimamo zilimpa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margareth Thatcher, lakabu ya mwanamke wa chuma (Iron Lady), Rais huyu wa kwanza mwanamke kwenye historia ya Tanzania ameonyesha pia moyo wa chuma.
Si siri kwamba kuna wahafidhina ndani ya CCM ambao hawapendezwi na dhamira yake ya kutafuta maridhiano ya kitaifa kisiasa. Kuna fununu kuwa baadhi ya viongozi ndani ya CCM wenye manung’uniko kinachoendelea kitawapa wakati mgumu kuchaguliwa ten ana wananchi katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.
Kundi hili linaundwa na wale wanaoamini kwamba kuchaguliwa kwao kwenye nafasi mbalimbali matokeo ya aina ya siasa zilizotamalaki Tanzania kati ya mwaka 2015 hadi 2020 na mabadiliko yoyote kurejea kwenye siasa za kistaarabu zinazoonekana kupendelewa na Samia ni hatari kwa mustakabali wao. Ikumbukwe kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 ulipingwa vikali na vyama vikuu vya upinzani na kukosolewa na baadhi waangalizi wa kimataifa kwa kupelea katika viwango vya uwazi, uhuru na haki.
Wapo pia wana CCM wanaojitanabaisha kama wafuasi wa U-Magufuli na mambo yanayofanywa na Rais Samia yanaonekana kung’oa hiba (legacy) ya kisiasa aliyoweka mpendwa wao huyo. Ni wazi kwamba Rais Samia anafahamu ukinzani wa makundi haya mawili lakini hilo halijazima dhamira yake ya kuendeleza maridhiano.
Kwa nini Samia anafanya anayofanya?
Mara baada ya Rais Samia kuingia madarakani, nilimuuliza Waziri wa sasa wa Nishati, January Makamba – wakati huo akiwa nje ya baraza la mawaziri, kunipa maelezo kidogo kumhusu. January alifanya kazi chini ya Rais huyo wa sasa wakati akiwa Makamu wa Rais wa Magufuli naye akiwa Waziri anayeshughulikia Muungano na Mazingira.
January alinieleza kwamba kwa maoni yake, Samia “is the most underrated politician in the country” (kwamba Samia ni mwanasiasa mahiri ambaye wengi hawampi heshima anayostahili). Mambo ambayo anayafanya sasa yanadhihirisha kauli hiyo ya Makamba.
Kitabia na kihaiba, Samia hafanani na Magufuli na asingeweza kufuata nyayo zake. Aina ya siasa ambazo anaweza kung’ara ni aina hii ya siasa anazofanya sasa na – nikinukuu maneno ya busara za kiafrika, akijua kwamba yeye ni samaki, ameamua kufanya siasa zake kwenye maji.
Kuna mambo mawili ambayo yanaonyesha kwamba siasa hizi za Samia ndiyo nguvu yake. Mosi ni ukweli kwamba aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye timu ya kwanza kabisa aliyoiunda kutafuta maridhiano ya kisiasa visiwani Zanzibar. Lakini wakati wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), alipewa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wake, akipewa jukumu la kuongoza baadhi ya mijadala mikali na yenye hisia kuhusu masuala ya haki za raia na Muungano.
Kuna pia suala la ushawishi wa chama. Wakati Samia anaingia madarakani miaka miwili iliyopita, nchi ilikuwa imegawanyika vipandevipande. Ushawishi wa CCM kwa raia wasio na vyama ulikuwa umeshuka na Magufuli alikuwa kama ndiye chama.
Kama Samia asingeleta siasa za mabadiliko, kulikuwa na hatari ya CCM kama chama kupoteza ufuasi na ushawishi na kubaki chama kinachotegemea dola kubaki madarakani. Hatua kama hizi za Samia kuzungumza na kukaa na wapinzani kunakipa CCM uhalali wa kuwa chama kiongozi na pia kukipa chama chake watu ambao kwa kawaida walikuwa hawana chama.
Huu unaweza kuwa mkakati mzuri kwa uchaguzi ujao wa mwaka 2025. Ingawa kuna muda mrefu kati ya sasa na wakati huo, kama hali itaendelea kuwa hivi ilivyo sasa, itakuwa vigumu sana kwa CCM kushindwa kwenye uchaguzi huo.
Chadema inapata au inapoteza?
Machapisho mbalimbali ya kisomi kuhusu siasa za Afrika yanaeleza kuhusu sababu kubwa mbili zinazoweza kufanya mabadiliko ya uongozi kutoka chama tawala kwenda cha upinzani; uhusiano baina ya tabaka tawala na uwezo wa kufanya vurugu.
Mara nyingi, upinzani unaweza kuingia madarakani pale ambapo uhusiano baina ya tabaka la utawala ni wa kuaminiana na pande zote zinaweza kufanya vurugu zenye maafa makubwa kwa upande pinzani.
Mfano mzuri ni jirani wa Tanzania, Kenya. Rais Ruto kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa chama kimoja na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta na mpinzani wake sasa, Odinga. Wanasiasa wengine mashuhuri kama Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Eugene Wamalwa na wengine wamewahi kuwa – kwa nyakati tofauti, ama chama kimoja au vyama tofauti. Kwa hiyo tabaka la watawala la Kenya linafahamiana na kuaminiana.
Kwenye uwezo wa kufanya vurugu, Ruto anaweza kutumia ngome yake ya eneo la Bonde la Ufa lakini Raila anaweza pia kwa kutumia ngome yake ya Nyanza na Mudavadi na Kalonzo kupitia kwao. Kwenye vurugu zilizotokana na uchaguzi wa mwaka 2008, pande zote ziliumizwa na kilichotokea. Kwa sababu hiyo, hakuna mwenye ukiritimba wa vurugu.
Hali hiyo ni tofauti na nchi kama Uganda ambako uhusiano wa tabaka la watawala na kuaminiana hakupo na hakuna wa kushindana na Museveni kwenye uwezo wa kufanya vurugu. Hali iko namna hiyo nchini Rwanda na Zimbabwe.
Baada ya miaka saba ya Magufuli, kazi ya kwanza kwenye kurejesha nchi ilipokuwa ni kurejesha uhusiano mwema na kuaminiana miongoni mwa tabaka la watawala. Tanzania ilikuwa imefika mbali kwenye hatua hii ambako kufikia mwaka 2016, Chadema ilikuwa na mawaziri wakuu wastaafu wawili – Edward Lowassa na Frederick miongoni mwa wajumbe wake wa Kamati Kuu.
Pengine huu ndiyo mchezo wa kisiasa unaochezwa na Chadema sasa na hatua kubwa itakayofuata itakuwa ni kujaribu kutafuta uwiano wa ukiritimba wa vurugu ambako kwa sasa CCM ina faida kuliko vyama vingine.
Na hakuna hatua kubwa kwenye jambo la kwanza kama kuwa na Rais kwenye mkutano wako. Kwa leo, Chadema na Rais Samia wamecheza mchezo ambao utawasaidia kwenye mkakati wao wa muda mrefu kisiasa.
Kwenye mchezo wa mpira wa miguu, tungesema matokeo leo ni 1-1.




Post a Comment