MOTO WAANZA KUWAKA UGANDA, SITA WATIWA MBARONI KWA USHOGA
Siku moja tu baada ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuwahutubia wabunge wanaojiandaa kuujadili na kuupitisha muswada wa sheria kali dhidi ya vitendo vya kishoga, wanaume sita wamekamatwa wakidaiwa kufanya ushoga.
James Mubi ambaye ni msemaji wa jeshi la Polisi, alisema kuwa wanaume hao sita walikamatwa wakiwa wamejifungia katika chumba kimoja huko Jinja, wakifanya ushoga.
Alisema kupitia mtandao maalum wa kijasusi, waliweza kubaini uwepo wa watu hao, hasa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo katika mji huo ulio mashariki mwa Mji Mkuu Kampala kwa umbali wa km 80.
Jana Ijumaa, Rais Museveni aliwaambia wabunge kuwa watu wanaojihusisha na ushoga ni waliopotoka na kwamba jamii yao wala ile ya imani ya kikristo haikubaliani na jambo hilo.
Uganda ni taifa la kwanza Afrika Mashariki kupinga ushoga waziwazi na kuutungia sheria kali, licha ya wito wa nchi za Magharibi kuutetea kwa hoja ya haki za binadamu.

Post a Comment