MIAKA MIWILI BILA JPM, WATANZANIA WAGAWANYIKA WAKIMZUNGUMZIA
Wakati Tanzania ikitimiza miaka miwili tangu kifo cha rais waka wa awamu ya tano, wananchi wamegawanyika kimtazamo kuhusu aina na namna ya uongozi wa Hayati John Pombe Magufuli maarufu kama JPM.
Rais Magufuli alitangazwa kufariki Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.
Jana Machi 17, 2023 alikuwa anatimiza miaka miwili ya umauti na shughuli mbalimbali za kumbukizi zimefanyika maeneo mbalimbali, ikiwemo ibada maalum iliyoongozwa na Mwadhama Kardinali Policarp Pengo iliyofanyika kaburini kwake, Chato.
Hata hivyo, ukiondoa wanasiasa wa upinzani ambao wamekuwa wakimshutumu kwa uongozi wake, wananchi wengi wa kawaida wamegawanyika, wanaomsifu na wanaokataa utendaji wake.
Hata hivyo, uchunguzi usio na shaka wa blog hii umebaini kwamba watu wengi wanaomkashifu na kubeza uongozi wa JPM wanafanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii, tena wote wakitumia majina bandia.
Na wale wanaomsifu, wanafanya hivyo kwa kutumia vyombo vya habari vya wazi.
Kwa maana hiyo, upo uwezekano mkubwa kwamba walewale wanaomponda katika mitandao ya kijamii, ndiyo haohao wanaomsifu katika vyombo vya habari.
Lakini lililo dhahiri ni kuwa wananchi wa Tanzania hawaimbi wimbo mmoja linapokuja suala la aina ya uongozi wa JPM.
Wapo wanaomuunga mkono, wakisema ni kiongozi aliyekuwa jasiri, asiye na woga na mwenye uthubutu. Kwamba alirejesha nidhamu ya watumishi serikalini na akaondoa njia nyingi za upigaji wa pesa za serikali.
Kwamba alikuwa na nia njema na nchi, kwani alianzisha miradi mikubwa ya kimkakati iliyolenga kuongeza pato la taifa na kupunguza mzigo kwa wanancbi.
Wanaompinga wanasema JPM alikuwa haambiliki, hashauriki na muoga kwani hakuruhusu mawazo mbadala na yeyote aliyetofautiana naye mawazo alikuwa adui yake.
Wanasema kiongozi huyo aliwachukia matajiri na kutumia kigezo cha ukwepaji kodi kuwarudisha nyuma na mbaya zaidi, aliwatengeneza watu waliopindisha sheria makusudi ili kujinufaisha.

Post a Comment