MORRISON, KISINDA BYE BYE YANGA
Wachezaji wawili wa kimataifa wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, Mghana Bernad Morrison na Mkongomani Tuisila Kisinda watapewa mkono wa kwa heri mwishoni mwa msimu huu.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema wachezaji hao wawili ambao awali walikihama kikosi hicho kabla ya kurudishwa, wameshindwa kuonyesha ubora uliotarajiwa.
"Tuliwarudisha tukiamini katika uwezo wao, tulijua kuna kitu wangeongeza katika kikosi, lakini bahati mbaya wameshindwa, tutawaruhusu wakaendelee na maisha sehemu nyingine, sisi itabidi tutafute wengine wa kutufikisha kwenye malengo yetu," alisema mmoja wa mabosi wa Yanga, aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Badala yake, wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, wanamuangalia kwa karibu winga wa As Real Bamako ya Mali, Cheickan Diakite ambaye alicheza vizuri katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo, ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1 jijini Bamako nchini Mali.
Alisema wanataka kumuona tena katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumatano inayokuja, ili kujiridhisha kama winga huyo mwenye umri wa miaka 18 ndiye yuleyule aliyesumbua katika mchezo wa kwanza.

Post a Comment