MBAPPE NAHODHA MPYA UFARANSA

Mshambuliaji wa Paris St-Germain Kylian Mbappe ameteuliwa kuwa nahodha mpya wa Timu ya Taifa ya Ufaransa. Mbappe anarithi mikoba ya mlinda mlango wa Tottenham, Hugo Lloris, ambaye alistaafu soka la kimataifa Januari mwaka huu.

Mbappe, 24, ameichezea Ufaransa michezo 66 tangu alipocheza mechi yake ya kwanza mwaka 2017.

"Kylian anakidhi vigezo vyote vya kuwa na jukumu hili," kocha wa timu ya Ufaransa Didier Deschamps alikiambia kituo cha televisheni cha Ufaransa TF1 katika mahojiano yatakayorushwa Jumapili.

Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) lilithibitisha kuwa Deschamps amemteua Mbappe kama nahodha na mshambuliaji wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann kama nahodha msaidizi.

Mbappe alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana alipoisaidia Ufaransa kufika fainali ya pili mfululizo ya Kombe la Dunia, ambapo walifungwa na Argentina.

Alifunga mabao mawili kwenye fainali ya 2018 dhidi ya Croatia na alitajwa kuwa mchezaji bora chipukizi wa michuano hiyo huku Ufaransa wakitawazwa mabingwa wa dunia kwa mara ya pili.

 

No comments