HOMA YA MARBURG TANZANIA: WHO KUTUMA TIMU YA DHARURA YA WATAALAMU KAGERA
Shirika la Afya Duniani (WHO) linatuma timu ya dharura mkoani
Kagera nchini Tanzania kufanya uchunguzi zaidi wa magonjwa ya mlipuko kufuatia
mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD) wa kwanza kabisa nchini humo.
Dkt. Matshidiso
Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika alisema juhudi za mamlaka za afya za
Tanzania kubaini chanzo cha ugonjwa huo ni kielelezo tosha cha dhamira ya dhati
ya kukabiliana na mlipuko huo.
"Tunafanya kazi
na serikali kuongeza kasi ya hatua za kudhibiti na kukomesha kuenea kwa virusi
na kumaliza milipuko haraka iwezekanavyo," alisema katika taarifa
iliyotolewa Machi 21, 2023.
Timu ya dharura ya
wataalamu wa WHO itaangazia kutafuta visa katika jamii na vituo vya afya vya
mkoa huo ili kubaini muingiliano zaidi na kutoa huduma zinazofaa.
Wizara ya Afya
nchini Tanzania ilithibitisha kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika Wilaya
ya Kanda ya Ziwa ya Bukoba Jumanne tarehe 21 Machi 2023, takribani siku 4 baada
ya taarifa za "ugonjwa usiojulikana" kusambaa na kuua watu watano
akiwemo mhudumu wa afya.
Watu hao kabla ya
kufariki walipatwa na dalili za homa, kutapika, kutokwa na damu kutoka sehemu
mbalimbali za mwili na figo kushindwa kufanya kazi. Serikali inasema kwa sasa
inafuatilia watu 160 ambao wanaweza kuwa walichangamana na watu walioambukizwa.


Post a Comment