IJUE FAMILIA YA TUZO TANZANIA, MBILI ZIMETOLEWA NA MALKIA WA UINGEREZA, MOJA NA RAIS WA TANZANIA
Kila mtu au familia ana karama zake mbele ya Mwenyezi Mungu, ingawa pia bidii, maarifa na uaminifu kazini huongeza thamani ya unachokifanya.
Mzee Paul Peter Kimiti, ni mwanasiasa mkongwe aliyehudumu kwa miaka mingi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi mbalimbali, tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwaka 1988, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi alimpa Paul Kimiti Tuzo au Nishani ya Jamhuri kwa utumishi wake uliotukuka, tangu alipoajiriwa kwa mara ya kwanza mwaka 1969.
Lakini pia alipewa Tuzo nyingine na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, AbdulWakil Juma ya Umoja wa Vijana mwaka huohuo, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Lakini familia yake ni kama familia ya tuzo kwani mwaka 1954, baba yake, Petro Kimiti alipewa Tuzo ya Utumishi uliotukuka. Alipewa tuzo hiyo na Malkia Elizabeth, miaka miwili tu baada ya kushika wadhifa huo.
Mzee Petro Kimiti alikuwa ni dereva, akiwaendesha Mkuu wa Wilaya na Gavana mkoani Sumbawanga.
Kana kwamba haitoshi, mwanae wa pili ambaye anafanya kazi katika Mamlaka ya Mapato nchini Uingereza, akiwa na makazi yake Cardiff huko Wales, Prudensi Kimiti mwaka jana alipewa tuzo na Malkia ya MBE, ya kutambua mchango wa utumishi wake kwa umma wa waingereza.

Post a Comment