HOMERA ATAKA WANAOTENGENEZA MAGARI YAO TAMESA KULIPA MADENI YAO

Na. Alfred Mgweno (TEMESA Mbeya)

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amezitaka Taasisi za Serikali zilizoko Mkoani Mbeya kuanza kutengeneza magari ya Taasisi zao na mitambo katika karakana za Wakala huo kwani kwa sasa umejizatiti na uko tayari kusimamia huduma hizo kwa weledi na ufanisi mkubwa. 

Homera ameyasema hayo Tarehe 10 Machi, 2023 wakati wa kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana ya TEMESA Mbeya kilichofanyika Karakana ya Wakala huo iliyoko eneo la Sabasaba kata ya Mbalizi mjini Mbeya.

Akizungumza katika kikao hicho cha wadau, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya  Juma Homera ametoa wito kwa Taasisi zote za Umma kuendelea kutumia huduma za Wakala huo kwani kwa sasa TEMESA iko vizuri na imejipanga vizuri.


 ‘’Kulikua na fikra huko nyuma, ukiangalia TEMESA ukipeleke gari unasema kwamba hali ni mbaya, lakini sasa TEMESA ya Awamu ya Sita ni TEMESA ya vitendo, hongera sana TEMESA kwa mabadiliko haya nimeshuhudia kwa macho yangu vifaa vya kisasa vimefungwa hapa, sasa naagiza Taasisi zote za Umma njoeni mtengeneze magari yenu hapa, watakadiria na watatengeneza kwa weledi wa hali ya juu sana, vinginevyo tutaendelea kupata hasara kwa kupeleka magari yetu mitaani  ambako wanatengeneza magari ndani ya siku mbili tatu yanaharibika, hapa wana mitambo mizuri, na wana vitendea kazi na vifaa vizuri na vya kisasa ambavyo wamewezeshwa na Serikali."

Homera pia amewashukuru wadau hao kwa kujitokeza kwenye kikao hicho ili kutoa mrejesho wa huduma wanazopatiwa na kusema kuwa  uwepo wake katika kikao hicho si wa bahati mbaya bali amefika hapo kwa ajili ya kuangalia ufanisi wa TEMESA kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. 

"Hii inatuonyesha kwamba TEMESA ile ya Awamu zingine sio sawa na ya Awamu ya Sita, ni TEMESA tofauti kidogo ndio maana tumekuja kuangalia vifaa walivyonavyo na tumeshuhudia kwamba mabadiliko ni makubwa, kwahiyo kipekee kabisa tumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuibadilisha TEMESA na kuwa TEMESA ambayo imebadilika sana kwa usimamizi mkubwa wa ndugu yetu Lazaro Kilahala, mimi niseme tu kwamba Mhe. Rais ameweka zaidi ya shilingi milioni 700 kwenye ununuzi wa vifaa nchi nzima, haya ni mafanikio makubwa sana na tumpongeze sana Mhe. Rais.’’ alisisitiza.

"Lakini pia nisisitize, wadau tulipe madeni, kama tulivyoambiwa kwenye hotuba, TEMESA anadai Taasisi za Umma Zaidi ya shilingi Bilioni 3.8, na wakati huo huo wanadaiwa na wazabuni Bilioni 3.7, hiki ni kiasi kikubwa sana kwa Taasisi ya Umma kudaiwa, hivyo niombe wale wote wanaodaiwa  andika barua uki waorodhesha na majina ya Taasisi zao, leta tuanze kuwaandikia barua ili walipe hayo madeni." alisema.


No comments