BASI LAPOKWA LESENI KWA KUCHEZEA KIFAA CHA KUDHIBITI MWENDO, LATRA YATOA AGIZO
Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) umesitisha leseni ya basi la kampuni ya Matarama Luxury linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Kahama kwa kosa la kuchezea kifaa cha kudhibiti mwendo kijulikanacho kwa kitaalamu kama VTD.
Katika taarifa yake kwa umma leo,LATRA imesema basi hilo lenye namba za usajili T835EBR lilifanyiwa uchunguzi Februari 28 mwaka huu na kubainika kuwa kifaa hicho kinachotoa taarifa ya mwendokasi wa gari kimechezewa na hivyo kushindwa kutoa taarifa sahihi.
Uchunguzi buo ulifanywa kwa pamoja kati ya mamlaka hiyo na kampuni inayofunga vifaa hivyo, Easy Track Solutions.
LATRA imesema kwa mujibu wa kanuni ya 27(2) ya leseni za usafirishaji ya mwaka 2020, inasitisha kwa muda leseni hiyo na mmiliki wa basi hilo kulazimishwa kufanya yafuatayo.
Kwanza anatakiwa kuwasiliana na kampuni inayofunga vifaa hivyo ili kukirejesha kifaa kilichochezewa katika hali yake ya kawaida na kisha atatakiwa kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa agizo hilo.

Post a Comment