BAA LA NJAA KENYA, WATOTO WACHINJA MBWA NA KUMLA HADHARANI, WAZAZI WAPANGA FOLENI CHAKULA CHA WANAFUNZI

Pengine haisemwi kwa ukubwa unaostahili, lakini ukweli ni kwamba hali ni mbaya sana kwa majirani zetu Kenya, kuna ukame na uhaba mkubwa wa chakula.

Katika eneo la kati la nchi hiyo, ripoti zinasema hakuna mvua kwa misimu sita mfululizo sasa, hali inayosababisha ukosefu wa chakula kwa kuwa hakilimiki, maji ya kunywa binadamu na mifugo imekuwa ikifa kwa makumi kila siku.

Katika sehemu za Seisei, Baragoi huko Samburu Kaskazini, watoto wenye umri wa kati ya miaka minne hadi nane, walilazimika kumkamata mbwa mdogo mwenye umri wa miezi sita, kabla ya kumchinja, kumchoma na kumla ili kikabiliana na njaa iliyowasumbua kwa muda mrefu.

Tukio hilo limethibitishwa na Naibu Kamishna wa Samburu, Jackson Oloo ambaye licha ya kukiri, lakini aliwaomba wananchi kuacha kula vyakula ambavyo kwa kawaida binadamu hawali, ili kujinusuru na madhara ya kiafya.

Hali ya ukame inayatesa maeneo mengi nchini Kenya na vyakula vinavyotolewa kama msaada haviwafikii maelfu ya wakenya wanaoishi maeneo ya vijijini ambayo yameathiriwa kwa kiwango kikubwa.

Siku kadhaa zilizopita watoto wawili wa familia moja waliripotiwa kufa kwa njaa huku maelfu ya watoto wengine wakiwa hawajiwezi majumbani.

Huko katika Kaunti ya Kajiado, msururu wa wazazi umeonekana ukipanga foleni na wanafunzi, wakisubiri kupewa chakula ambacho wanafunzi wanapewa bure.

Wanaume na wanawake wamekuwa wakiingia misituni kusaka mizizi kwa ajili ya chakula, mingine ikielezwa kuwa ni sumu. Licha ya wito wa viongozi wa serikali kutaka wakenya kutotumia mizizi na vyakula vya wanyama wasioliwa, lakini dalili za kupata misaada ni ndogo, hivyo wengi wanamudu kuishi kwa mizizi na kula wanyama kama mbwa na paka ambao kwa kawaida hawaliwi.

No comments