NINI WACHINA, NJOO MBINGA WATU WANAPIGA UGALI KWA KIJITI, TENA ASUBUHI!
Waliofika kule Uchina wanatuambia wale jamaa wanakula vyakula vyao kwa kutumia vijiti na hata hapa nchini, wakiwa katika migahawa yao, unaona jinsi vijiti vinavyochukua nafasi ya vijiko.
Sasa kama hilo huwa linakushangaza, utashangaa zaidi ukisikia hii kutoka Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma ambako watu kwa mamia, kila siku wanakula ugali kwa kutumia vijiti.
Katika eneo maarufu liitwalo Manzese mjini hapo, nyama choma, utumbo na ugali ni vyakula vinavyoliwa kila siku kwa vijiti, na cha kuvutia zaidi, inapofika saa saba mchana, biashara huwa imeisha.
Wachomaji wa nyama ambao ni wanaume, huwa wanakuwa na mpishi wao anayepiga ugali. Wateja wakinunua nyama inayouzwa kuanzia kipande cha shilingi elfu moja,hula kwa pamoja.
Muuzaji atakatakata vipande halafu ataviweka juu ya jiko, watu wote waliopo pale watakula kwa kutumia vijiti.
Wanaweza kuwa hata wateja kumi,kila mmoja kwa kiasi alichoagiza,nyama itachomwa na kukatwakatwa na kuweka kwenye wavu jikoni na wote watakula na ugali na mboga za majani.
Biashara hii inaanza saa tatu asubuhi na inapofika saa saba za mchana, nyama zote, kutoka kwa karibu wauzaji zaidi ya kumi waliozunguka eneo hili wanakuwa wamemaliza.
Nyama choma, utumbo na mboga za majani ikiliwa na ugali, inachombezwa na pilipili iliyotengenezwa kwa nyongo kwa kukamuliwa na limao.

Post a Comment