NILITEMBEA MASÀA MATANO UMBALI WA NUSU SAA, KISA NILIPINGA HAKUNA UCHAWI
Nipo kijijini kwetu, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Nimekaa na marafiki zangu wa utotoni tunakunywa pombe ya kienyeji maarufu kama Ulanzi.
Hali ya hewa ni joto, sio joto kama la pwani, isipokuwa kwa kawaida huku ni baridi, muda wote watu wanavaa makoti, masweta au mashati mawilimawili. Sasa inapotokea mtu akavaa tu shati, maana yake ni joto.
Tumekutana jioni hiyo kwa stori mchanganyiko, kila mmoja analeta yake. Hata hivyo stori nyingi ni za kusengenyana, kila mtu anasimulia mabaya ya asiyekuwepo!
Jioni hiyo tulikuwa tumetoka msibani, kumzika mwanakijiji mwenzetu ambaye alifarki baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Hata sijui ilikujaje, mara mtu akaanza kusema kuwa marehemu ambaye alikuwa na umri wa miaka 45, aliuliwa na baba yake ili alipe madeni.
Ngoja nikueleweshe. Huku kwetu wachawi wake ni wa ajabu kidogo. Wao huua ili wale nyama. Kifupi wachawi wa kwetu wanakula nyama ya binadamu!
Sasa ikitokea kwa mfano mimi nimemuua mtoto wangu (lazima uue mtu wa damu yako), usiku nitaigawa nyama ile kwa wachawi wenzangu ambao kimsingi wanakopa. Na kama nilikopa huko nyuma, basi hapa nitalipa.
Ukikopa kidole gumba mkono wa kulia, utapaswa kulipa kidole gumba mkono wa kulia. Hivyo hivyo kwa viungo vyote vya binadamu.
Sasa huyo jamaa ndiyo akasema baba mtu alimuua kijana wake ili alipe madeni maana alikuwa anadaiwa sana. Mimi,ingawa nasikia utamaduni huu kwa miaka mingi, lakini nimegoma kuuamini.
Nikawa nabisha, nawaambia hakunaga wachawi, isipokuwa mbwembwe tu. Robo tatu ya watu tuliokuwa kilingeni,walikubaliana uwepo wa uchawi, waliobaki walikaa kimya na aliyepinga ni mimi peke yangu.
Sasa tumepiga stori pale hadi ilipofika saa mbili usiku, nikainuka nirudi nyumbani, umbali ambao kila siku hutumia nusu saa. Na huku sijakuzoea kivile kwa maana hiyo narudi mapema.
Sikuaga, ila nilifanya kama naenda jisaidia haja ndogo,nikapotea mazima.
Nimetembea umbali wa kutosha,nikashtuka. Ni kama nimetumi muda mwingi halafu sifiki?
Nikatazama muda katika simu, ni saa tatu usiku. Mbona kule nimeondoka saa mbili? Nikajishangaa mwenyewe.
Nikaongeza mwendo na kuwa makini na saa. Pale niliposhtuka wala hapakuwa na umbali kutoka tulipokuwa tunakunywa. Sasa kila nikipiga hatua, naenda mbele lakini ni kama narudi nyuma.
Amini usiamini, saa tano usiku hata nusu ya safari sikuwa nimefika. Kwa
mara ya kwanza katika maisha yangu,nikapatwa na hofu ya uchawi!
Ajabu sasa, kwa muda wote niliokuwa natembea sikukutana na mtu, si anayekwenda au anarudi, jambo ambalo si la kawaida maana hiyo njia ninayopita ni njia kuu!
Nikatoa simu yangu na kumpigia mdogo wangu mmoja mwenye piipiki ili aje anichukue. Simu yake haikupatikana, nikawapigia na madogo wengine watatu, nao hawakuwa hewani.
Kwa muda ule wa saa tano usiku, huku kijijini ni kama usiku wa manane. Nikajaribu kukimbia, sikuweza, pumzi na ile pombe niliyokunywa ningeweza kuanguka. Nikajitahidi kukaza mwendo, lakini dhahiri, sikuwa natembea mwendo niutakao!
Nilifika nyumbani saa saba usiku, kitu ambacho sijawahi kukifanya, maana huku kijijini, watembeao usiku ni wenyeji.
Sikulala, asubuhi na mapema nikamwendea kijana mmoja ninayemfahamu vizuri, alutekuwepo jana wakati tunajadili uchawi, nikamsimulia kilichonitokea.
Alicheka sana, akaniambia jamaa wamejaribu kunionyesha kwa vitendo kuwa uchawi upo na akanitajia aluyenifanyia mchezo huo.
Nikarudi nyumbani na kukusanya vitu vyangu, nikachukua bodaboda hadi Mbinga mjini, kesho yake nilikuwa ndani ya basi nikirejea Dar.
Sina uhakika kama nitarudi tena kwetu au la, ila hadi sasa sijamuambia mtu ye yote!!!!

Post a Comment