KAMA UDAKTARI WA MUZIKI ANGEPEWA PROFESA JAY

Jana Mbunge wa Morogoro Kusini, Hamis Tale, maarufu kama Babu Tale, aliibua gumzo baada ya kuliambia Bunge kuwa yeye ni PHD Holder, hivyo atambukiwe kama daktari.

Baada ya kauli hiyo, yalifuata majadiliano makali, yaliyomuibua Spika Tulia Ackson ambaye alipigilia msumari wa moto kwa kutaka uwezo wa uangalizi kwa namna shahada hizo zinavyotolewa holela nyakati hizi.

Baada ya mashambulizi mengi kutoka kwa wabunge wenzake na baadaye wadau, mwenyewe alipata nafasi ya kujibu alipokutana na waandishi wa habari baadae.


Babu Tale alisema yeye ameupata udaktari huo kutokana na fani yake, kwani hakuna siri kuwa zaidi ya wasanii 50 wamepita katika mikono yake, akiwa kama kiongozi mwelekezi,

Aidha, amesema pia ametengeneza mmoja kati ya walipa kodi wakubwa vijana ambaye anaweza kushika moja kati ya nafasi tano za juu, bila shaka akimaanisha Diamond Platnumz!

Kabla ya kuwa mbunge, Babu Tale alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa kundi la Tip Top Connections, lenye wasanii kadhaa maarufu, chini ya Madee, Tundaman, Keisha, Dogo Janja kuwataja kwa ufupi.

Katika kundi hilo, alishirikiana na kaka yake marehemu Abdul Bonge. Baadaye alichukuliwa na Wasafi akiwa mmoja kati ya mameneja watatu, wengine wakiwa ni Sallam na MKubwa Fella.

Sitaki kubeza mchango wa Babu Tale katika sanaa ya muziki wa kizazi kipya, lakini pia sidhani kama anastahili heshima ya kuitwa daktari kwa maana ya mchango wake uliotukuka.

Tale alikuwa kiongozi enzi zile za ujima wa wasanii, ambako Meneja ndiye alikuwa juu ya msanii na angefanya lolote pasi na woga.

Wasanii walikuwa waoga kudai haki zao kutokana na mfumo. Hawa mameneja ya staili ya Tale walikuwa viungo kati ya walioshika muziki na wasanii, wao ndiyo wakipanga bei za kulipwa.

Ni kipindi cha akina Tale ndicho wasanii walikuwa tayari kupanda jukwaani kwa kiasi chochote cha pesa ili mradi waonekane.

Leo anasema vijana zaidi ya 50 wamepitia mikononi mwake, lakini ukimwambia awataje wangapi kati ya hao walikuwa angalau na nyumba yeye akiwa meneja wao sina hakika kama tutawapata angalau watatu.

Kama kuna mtu anastahili udaktari wa heshima kwa mchango wake mkubwa katika Bongo Fleva, basi ni mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay,

Huyu alileta mageuzi ya kweli ya muziki huu, akiutoa kutoka kuonekana wa kihuni na kuwafanya watu wazima waanze kuamini kuwa yaweza kuwa ajira.

Ndiye aliyewafanya ndugu, jamaa na marafiki kuanza kuwaruhusu vijana wao kujihusisha na Bongo Fleva ambayo mwanzoni ulionekana muziki wa wahuni, wavuta bange na waliofeli maisha.

Sio ajabu, vijana wote 50 waliopitia mikononi mwake, wote ni zao la Profesa Jay ambaye alikuwa bora katika uandishi wa mashairi yenye staha, yanayofundisha huku yakiburudisha.



No comments