BILIONI SABA UNUSU KUIKARABATI MV MAGOGONI KIGAMBONI
Serikali itafanyia ukarabati wa kivuko kinachotoa huduma ya usafiri majini eneo la Kigamboni cha MV Magogoni, kwa thamani ya shilingi za Kitanzania bilioni 7.5.
Hayo yanafuatia utiaji saini uliofanywa jijini Dar ea Salaam, ambapo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA), Lazaro Kilahala aliiwakilisha serikali na Mkandarasi, African Marine and General Engineering Company Ltd yenye makazi yake Mombasa nchini Kenya.
Tukio hilo lilishuhudiwa pia na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Spika, Mussa Hassan Zungu na Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndungulile.
Waziri Mbalawa alisema ni dhamira ya serikali kuona kuwa miundombinu ya usafiri wa majini inaboreshwa ili iweze kurahisisha na kuharakisha shughuli za kiuchumi katika wilaya za Kigamboni na Ilala na maeneo ya jirani.
Mtendaji Mkuu wa Tamesa, Lazaro Kilahala awali, alisema ukarabati huo utafanyika katika maeneo mengi ya kivuko hicho ikiwemo mfumo wa umeme, uwekwaji majenereta mapya, sehemu ya uongozaji kivuko, mfumo wa tahadhari ya moto na mengine.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 500, sawa na abiria 2000 na magari madogo 60, kitaanza kukarabatiwa mwezi ujao na abiria wametakiwa kutumia zaidi usafiri wa magari unaopitia daraja la Nyerere.

Post a Comment