WAKUBWA WALIPOKA UDIWANI WANGU

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mkumbi mwaka 2015 hadi 2020, Tomas Vitus Kapinga amedokeza kuwa nafasi yake hiyo ilipokwa katika uchaguzi uliofuata kutokana na viongozi wawili wakubwa wa wilaya ya Mbinga kumkomoa kutokana na msimamo aliokuwa nao kwa wapiga kura wake.

Katika mahojiano na Ojuku Blog yaliyofanyika leo Jumatano ofisini kwake mjini Mbinga, Kapinga amesema alikuwa na msimamo usioyumba akipinga mpango wa kupeleka makao makuu ya Halmashauri ya Mbinga Vijijini huko Kiamiri.

Alisema viongozi hao ambao majina yao yanahifadhiwa kwa sasa kwa kuwa hawakupatikana kujibu tuhuma hizo, waliwatumia wenyeviti wa vijiji vinavyounda kata yake kuhakikisha wanamuhujumu ili jina lake lisipite wakati wa kura za maoni mwaka 2020.

"Nilikuwa na msimamo imara sana kupinga halmashauri kwenda Kiamiri, kwani kijiografia, eneo hilo liko mbali na wananchi wa Mbinga vijijini, ambao ili kufika wanalazimika kuipita kwanza Halmashauri ya Mbinga Mji, ndipo uende Mbinga Vijijini.

"Lakini kama ingejengwa katika sehemu tuliyoomba sisi, wananchi hao wasingelazimika kuvuka halmashauri moja hadi nyingine. Niliwaongoza madiwani wenzangu watatu kwenda Dodoma kuonana na Rais Magufuli, jambo ambalo viongozi wa wilaya hawakulipenda kabisa."

Alisema Rais John Magufuli aliwakabidhi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jaffo ambaye aliteua kamati maalum ya kushughulikia suala hilo.

"Kabla kamati hiyo haijafika Mbinga, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa agizo la kutaka halmashauri hiyo kujengwa Kiamiri. Hii ilikuwa wakati wa ziara yake hapa Mbinga. Ninaamini kabisa alichukua uamuzi huo baada ya kushauriwa vibaya na hao viongozi," anasema Kapinga.

"Waliwatumia wenyeviti wa vijiji kunihujumu, mmoja walimtaka naye aingize jina lake, lengo ni kupunguza kura zangu maana nilikuwa nakubalika sana," alisema.

Kuhusu vitu anavyojivunia kuvifanya wakati wa uongozi wake, alisema kuanzisha miradi mitatu ya ujenzi ambapo mmoja ilikamilika kabla hajamaliza muhula wake.

Mradi huo uliokamilika ni wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mtawa ambacho wanakijiji waliamua kuiita zahanati hiyo kwa jina lake kutokana na kuthamini mchango wake.

Aidha, katika kijiji cha Majingo, aaliasisi ujenzi wa majengo ya shule ya msingi ambao hadi anaondoka ulikuwa bado unaendelea, Pia katika kijiji cha Longa, aliacha mradi wa ujenzi wa bweni la wavulana na nyumba ya patroni wa Shule wa Sekondari Lpnga.

Kuhusu changamoto alizozipata akiwa madarakani, diwani huyo mstaafu alisema ukiondoa mgogoro wa kimaslahi kati yake na viongozi hao wa wilaya, hakuwa na matatizo yoyote.

Akijibu swali kama kukosa udiwani kumehitimisha safari yake kisiasa, alisema bado ana nia ya kuwania nafasi zingine za uongozi, kwani anaamini jamii bado inahitaji msaada wake.

"Kuna watu wameshika nafasi lakini hawawajibiki ipasavyo, nataka kupata nafasi ili nishirikiane na viongozi wasomi wakiwemo wabunge tuweze kuisaidia jamii yetu kusonga mbele zaidi ya hapa tulipo."

Kuhusu nafasi anayotarajia kuiwania, Kapinga alisema atawania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi ili awanie Ubunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini.

No comments