RAIS SAMIA ASEMA TOZO NI KWA MAENDELEO, ZITAENDELEA KUWEPO

SIKU chache baada ya tozo za miamala ya fedha katika mitandao
ya simu kushuka kwa asilimia 30, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tozo
zitaendelea kuwepo na hataki kuficha hilo.
Akizungumza na wananchi wa Tegeta, jimbo la Kawe jijini Dar
es Salaam, amesema, "Tuliweka tozo kwenye mambo ya fedha za mitandao,
yamepigiwa kelele sana, nimesikia. Nimekaa na wataalamu tumepunguza 30%. Miezi
miwili tuliyoanza nayo tumekusanya kama Bilioni 60 na zimepelekwa kujenga Vituo
220 vya Afya"
"Januari tuna wimbi kubwa la
Watoto wanataka kuingia Sekondari, lakini pia kuna wapya wanaoingia Darasa la
Kwanza. Hakuna wa kutujengea ni sisi wenyewe. Fedha zitakazokusanywa Septemba
na Oktoba zitaenda kujenga madarasa zaidi ya 500"
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemuita kwenye gari Mbunge
wa Kawe aliyeadhibiwa na Bunge, Askofu Josephat Gwajima, jambo lililomfanya
ashangiliwe sana na wananchi.
Akiwa juu ya gari la Rais, Askofu Gwajima amesema wananchi
wa Kawe siyo tu wanampenda mama Samia bali wana mahaba naye.
Wakati hayo yakiendelea, helkopta za Polisi zinaonekana juu
ya anga katika kuhakikisha usalama.
Rais Samia amewataka wananchi waendelee kulipa kodi kwani
kodi ni kwa maendeleo ya taifa.
Rais Samia amesema anaelekea Bagamoyo katika mtiririko wa
uchukuaji picha ya filamu ya vivutio vya utalii wa Tanzania itakayozinduliwa
nchini Marekani na kuonyeshwa dunia nzima.

Post a Comment