SILAA AWAWAHI POLISI, ATINGA BUNGENI

MBUNGE wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa amefika katika Kamati ya
Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhojiwa baada ya jana Kamati hiyo
kutoa ombi kwa Spika wa Bunge Job, Ndugai kutaka akamatwe.
Kamati hiyo iliomba kukamatwa kwa mbunge huyo na kufikishwa
katika kikao cha kamati saa 4.00 asubuhi leo Ijumaa Agosti 27, 2021.
Silaa aliitwa kuhojiwa kwa mara ya kwanza katika kamati hiyo
Agosti 24, 2021 akituhumiwa kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Imedaiwa kuwa Silaa alifika saa 12.00 asubuhi leo katika
viwanja vya Bunge, eneo ambalo lina kinga ya kukamatwa na vyombo vya dola kwa
mujibu wa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Hata hivyo, kabla ya kuitwa kuingia katika kamati hiyo, Silaa
alikwenda moja kwa moja katika ukumbi wa Spika ulioko jengo la Utawala la Bunge
akiwa pekee yake bila kusindikizwa na askari kama ilivyokuwa Agosti 24, 2021
alipohojiwa kwa mara ya kwanza.
Pia, tofauti na alivyohojiwa kwa mara ya kwanza ambapo alifika
na lundo la vitabu na sanduku lenye nyaraka mbalimbali, leo amefika akiwa na
begi dogo jeusi la mkononi.
Hata hivyo, baada ya mwenyekiti wa kamati hiyo kuingia
ukumbini, Silaa alitoka nje na kukaa katika viti vya kusubiria wageni vilivyoko
kwenye jengo hilo.

Post a Comment