WAZIRI BASHUNGWA ATOA MIEZI MIWILI KWA CRB NA NCC KUUNDA MABARAZA YA WAFANYAKAZI
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza katika uzinduzi wa Baraza la Wafanyazi la Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) na Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara hiyo na Taasisi zake, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent
Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha
Amour anazisimamia Taasisi za Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na Bodi ya
Usajili wa Makandarasi (CRB) kuhakikisha zinaunda Mabaraza ya Wafanyakazi
ambayo yanaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya
mwaka 2004.
Bashungwa ametoa agizo hilo
Aprili 22, 2024 jijini Dodoma wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi la Mfuko
wa Barabara (RFB) na Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Wizara na Taasisi zake
ambapo ameagiza hadi kufikia Juni 30, 2024 Mabaraza ya Taasisi za NCC na CRB
ziwe zinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria.
“NCC pamoja na CRB kupitia
kwa Katibu Mkuu jipangeni nataka hadi kufika Juni 30 nipate taarifa ya Taasisi
hizi ziwe na Mabaraza ya Wafanyakazi na yanayofanya kazi”, amesisitiza
Bashungwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour akitoa maelezo ya mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara hiyo na Taasisi zake, uliozinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, jijini Dodoma.
Bashungwa amewataka wajumbe
wa Baraza la Bodi ya Mfuko wa Barabara kubuni na kuleta vyanzo vipya vya mapato
kwa dhumuni la kusaidia uwepo wa mapato ya kutosha na endelevu kwa ajili ya
usimamizi wa matengenezo ya barabara hapa nchini.
Bashungwa amesisitiza kwa
wajumbe wa mabaraza kutumia fursa ya uwepo wao katika mabaraza hayo kuhoji na
kutoa mapendekezo yatakayokuwa na mchango na kuzaa matunda katika kuiletea nchi
yetu maendeleo.
Vilevile, Bashungwa
amewakumbusha wajibu wa Baraza la Wafanyakazi ikiwemo Usimamizi wa Rasilimali
watu sambamba na kuwajengea weledi, ujuzi na uwezo kwa watumishi pamoja na
kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.
Aidha, Bashungwa ameziagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Makadiriaji Majenzi na Wabunifu Majengo (AQRB) kufuatilia miradi wanayoisimamia kabla ya tatizo kutokea pamoja na kushirikiana na kuchukua hatua kwa watu wanaokiuka maadili ya taaluma zenu.
Kuhusu mfumo wa ufuatiliaji
na tathimini, Waziri Bashungwa amewasihi Wakuu wa Taasisi kuboresha majukumu
yao ya kiutendaji kupitia mfumo huo ikiwemo kuongeza ufanisi na weledi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleeza kuwa Wizara pamoja
na Taasisi zake itaanza kutumia rasmi mfumo huu kuanzia tarehe 2 Mei, 2024
ambapo matarijio ya Wizara kupitia mfumo huo utaongeza ufanisi wa Wizara na
Taasisi zake na kupunguza matumizi ya fedha za Serikali na kuwezesha kuwa na
takwimu sahihi kati ya Wizara na Taasisi zake.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Bodi ya Mfuko wa Barabara ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Bodi hiyo Mhandisi Rashid
Kalimbaga ameeleza kuwa Baraza la wafanyakazi wa Bodi hiyo linajumuisha wajumbe
mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Vitengo, Wawakilishi wa Vitengo, Wajumbe wa
Halmashauri ya TUGHE tawi la Bodi, Mwenyekiti wa TUGHE kutoka Wizarani, Mjumbe
wa TUGHE Taifa na Mjumbe wa TUGHE Mkoa wa Dodoma.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi

Post a Comment