WANANCHI NAMTUMBO WATAKA TAARIFA YA MAPATO NA MATUMIZI

NA STEPHANO MANGO, NAMTUMBO
BAADHI
ya wananchi katika Kijiji cha Mchomoro kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya
ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wamemtaka Mwenyekiti wa Kijiji hicho ,Mtendaji wa
kijiji na Mhasibu wa kijiji hicho kuitisha mkutano wa hadhara na kuwasomea
mapato na matumizi ili kuwepo na uwazi wa fedha za wananchi
Wakizungumza
na timu ya waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho jana walisema kuwa ni
haki yao kupata taarifa ya maendeleo ya kijiji ikiwa ni pamoja na taarifa za
mapato na matumizi ya fedha ambazo zinatokana na michango yao na fedha kutoka
Halmashauri.
Mmoja
wa wanakijiji hicho, Faraji Said alisema kuwa toka viongozi hao wa kijiji
wachaguliwe mwaka 2019 wameshindwa kufanya mkutano wa hadhara na kuwasomea
mapato na matumizi kwa sababu ambazo wanazijua wenyewe hali ambayo inaleta
mashaka katika matumizi ya fedha za wananchi.
Said
alisema kuwa ipo mikutano ya dharura na mikutano ya kuidhinishiwa matumizi ya
fedha ambayo imekuwa ikiitishwa kwa lengo lake binafsi mwenyekiti na wenzake na
kulazimisha ajenda kuwa moja bila kupata ufafanuzi hali ambayo imekuwa ikizorotesha
maendeleo ya kijiji.
“Akiitisha
mkutano basi ujue kuwa anataka kuomba fedha za kuendeshea ofisi au anataka
kupata baraka za kuwafukuza wafugaji jamii ya wasukuma ambao hawajampa fedha
ambazo alikuwa anazitaka kutoka kwa wasukuma hao ambao wamekuwa wakilisha
mifugo yao katika maeneo ya kijiji”alisema Said.
Alisema
kuwa jamii ya wanamchomoro wanahitaji kupata haki zao lakini wamekuwa
wakikwamishwa na uongozi mbovu wa kijiji hicho ambao umekuwa ukijali zaidi
maslahi yao badala ya maslahi mapana ya wananchi.
Naye
Adam Chake alisema katika kijiji hicho walifanikiwa kujenga boma la Zahanati
mwaka 2019 ambapo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Chiristine Mdeme alipotembelea ujenzi
huo aliahidi Kutoa milioni moja, na hayati Rais Dk John Magufuli aliahidi Kutoa
milioni 100/= pia jumuiya ya hifadhi ya Mbarang’andu nao waliahidi Kutoa
milioni 8.947/= lakini mpaka sasa hatujapata taarifa kuhusu ujio wa fedha hizo
au matumizi yake.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Said Mohamed Mkalela alisema kuwa madai
hayo siyo ya ukweli na kwamba amepanga kufanya mkutano wa robo mwaka hivi
karibuni ili kuweza kutolea ufafanuzi.
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Namtumbo Evance Nachimbiya alisema kuwa katika
vikao vyake na viongozi wa vijiji na watendaji wa Halmashauri hiyo alielekeza
kutatua kero za wananchi kwa wakati na Kutoa taarifa za utendaji kazi kwa
wananchi ili wananchi waweze kufahamu serikali yao inachofanya.
Nachimbiya
alisema kuwa kuwasomea mapato na matumizi wananchi ni haki yao na sio jambo la
msaada kwa sababu hizo ni fedha zao kwani kutokufanya hivyo ni kwenda kinyume
na kanuni na sheria na hatua zinachukuliwa ili kubaini ukweli wa madai ya
wananchi kabla ya sheria kuchukua mkondo wake.

Post a Comment