WANAJUMUIYA YA MBARANG’ANDU WAIOMBA TAKUKURU KUCHUNGUZA MAPATO NA MATUMIZI YAKE
NA STEPHANO MANGO, NAMTUMBO
WANANCHI
ambao wanaizunguka jumuiya ya uhifadhi ya Mbarang’andu iliyopo wilayani
Namtumbio mkoani Ruvuma wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
nchini (TAKUKURU) kuchunguza mapato na matumizi ya jumuiya hiyo kwa kipindi cha
miaka mitano ili kuwepo na uwazi katika uendeshaji wa Jumuiya hiyo.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wakati wa uchaguzi wa wajumbe wapya wa jumuiya hiyo kutoka
katika vijiji ambavyo vinaunda Jumuiya hiyo vya Mchomolo, Kitanda, Likuyuseka
Maganga, Kilmasela, Nambecha, Songambele na Mtelemwahi, walisema wanashangaa
kuitishwa kwa uchaguzi bila wale ambao wanamaliza muda wao kusoma taarifa ya
utendaji kazi wa miaka mitano iliyopita.
Akizungumza
kwa niaba ya wananchi wa Kitanda, Abdul Andunje alisema kuwa Jumuiya hiyo ni
taasisi hivyo ina mali na madeni ambayo wamekuwa wakidaiwa na taasisi
mbalimbali hivyo ni vyema taarifa ya mapato na matumizi ya jumuiya hiyo
ikatolewa kwa uwazi ili unapofanyika uchaguzi mpya ikaeleweka utendaji kazi wa
wajumbe ambao wanamaliza muda wao.
Andunje
alisema kuwa ni kitu cha ajabu kuitisha uchaguzi bila kuelewa kwa kina
kilichofanyika katika miaka mitano iliyopita ili kujua mali zilizopo na
kinachodaiwa na sababu zake za kuwepo kwa hali hiyo.
Alisema
kuwa kuruhusu uchaguzi bila kujua utendaji kazi wa wajumbe waliopita katika
miaka mitano ni kuruhusu mianya ya ubadhirifu na wizi katika jumuiya hiyo
ambayo imekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka nchi za Ulaya na Marekani
ambao wanatembelea jumuiya hiyo na kufanya shughuli za uwindaji.
Naye
Erasto Gama kutoka katika kijiji cha Songambele alisema kuwa zipo shughuli za
utalii na uwindaji ambao unafanyika katika Jumuiya hiyo ambazo zinaiingizia
Serikali mapato na tozo mbalimbali hivyo ni muhimu uwazi ukawepo na wananchi kujua
ukweli huo kwa sababu ni mali yao.
Gama alisema kuwa
wajumbe ambao wanamaliza muda wao yapo ambayo wameyafanya katika utendaji kazi
wao wa kipindi cha miaka mitano ambayo yanatakiwa yasemwe ili kuwapa fursa
wananchi kujua kilichofanyika kwenye Jumuiya yao kitendo cha kuitisha uchaguzi
bila kutolewa taarifa kinazua taharuki kwa sababu nyuma yake kuna vitu
vinafichwa.
Alipotafutwa
Afisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Saimon
Sambalu ili aweze kuelezea kwa kina kinachodaiwa na wanajumuiya hakuweza
kupatikana kwa madai kuwa alikuwa vijijini kikazi.
Hata
hivyo kwa upande wake Afrikanus Challe ambaye ni Afisa Maliasili na Utalii wa
Mkoa wa Ruvuma alisema kuwa kabla ya baraza la Jumuiya kuvunjwa kunatakiwa
kuitishwe mkutano maalum ambao ajenda yake kubwa itakuwa kupeana taarifa za
utendaji kazi na kuvunjwa kwa baraza.
Challe
alisema kuwa kwa sasa taarifa ambayo anayo ni mchakato wa uchaguzi katika
vijiji ambavyo vinaunda Baraza la Jumuiya hiyo, sasa kama kuna dosari zozote
katika uundwaji wake ni lazima zifanyiwe kazi kwa uwazi na ukweli ili kuondoa
makando kando hayo na kwamba analifuatilia jambo hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi
.

Post a Comment