SGR KUTUMIA MIFUMO YA KISASA KUZUIA AJALI ZA TRENI

IMEELEZWA kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), unatarajiwa kuwekwa mifumo ya kisasa ambayo itasaidia kuzuia ajali ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa uendeshaji wa reli hiyo na ambao hautamruhusu dereva kuzidi ama kupunguza mwendo uliowekwa.
Hayo yamesemwa na Meneja
Msaidizi wa mradi wa reli ya Kisasa, kipande cha Morogoro
- Makutopora (Km 422) kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi
Christopher Mang’wela, wakati akizungumza na wahandisi kutoka Serikalini na Sekta
Binafsi ambao wametembelea mradi huo uliofika asilimia 61, jijini Dodoma, kwa ajili
ya kujifunza utekelezaji wa mradi kuanzia hatua mbalimbali zilizotekelezwa.
“Kama mnavyoona,
mradi umefika asilimia 61, na uendeshaji wake utakuwa ni wa kisasa kwani utawekwa
vifaa maalum vya kumuongoza dereva wa treni ili kuzuia ajali.”amesema Mhandisi Mang'wela.
Awali, akizungumza kwa
niaba ya wahandisi hao, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi
Patrick Barozi, ameeleza kuwa anaona nia ipo na uwezo kwa watanzania katika kusimamia
miradi mikubwa inayoendelea nchini huku tukiwa na usimamizi mdogo kutoka wenzetu
wa nje na hivyo kuwaleta wahandisi wetu katika mradi kutaongeza chachu ya kuchukua
zabuni nyingi za miradi mikubwa inayoatarajiwa kuanza na kuendelea hapa nchini.
"Tumetembelea mradi huu katika baadhi ya maeneo ambapo tumeridhishwa na mradi
huu na tumeona unaendeshwa vizuri kuanzia mwanzoni hadi hapa ulipofika kwani kupitia
mradi huu wahandisi wamejifunza mengi", amefafanua Mhandisi Barozi.
Aidha, Mhandisi Barozi ameongeza kuwa kupitia vipande vitatu vya utekelezaji wa
mradi huo, wahandisi wa hapa nchini wamepata utaaalamu wa kutosha na hivyo
kuweza kuisaidia Serikali kwa utekelezaji wa awamu zinazofuata endapo watawezeshwa
katika suala zima la upatikanaji wa vifaa.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Mhandisi, Dkt. Ramadhan Mlinga, amesema kuwa wahandisi waliopo kwenye mradi huo
kufuatilia kwa makini kipindi cha mwisho cha utekelezaji wa mradi huo kwani kipindi
hiki husaidia kuboresha utekelezaji wa miradi inayofuata kwa kuangalia changamoto
zilizowakabili katika utekelezaji wa mradi uliopita na kutafutia ufumbuzi katika
utekelezaji wa mradi ujao.
"Kwa kawaida miradi ina hatua tano za utekelezaji ikiwemo kuibua mradi,
kupanga jinsi ya kutekeleza mradi, utekelezaji wa mradi, ufuatiliaji wa utekelezaji
wa mradi na kufunga mradi ambapo hivi ni lazima vizingatiwe ili mradi ufanikiwe”,
amesisitiza Mlinga.
Naye, Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Nyandalo Hezron,
amesema kuwa wamefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamewasaidia kujua uhalisia wa
yale waliyojifunza darasani na kuyaleta katika utekelezaji ambayo yawakumbusha miongozo
mbalimbali katika usimiamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayoendelea.
Mradi wa Reli ya Kisasa
(SGR) ulioanza mwezi Aprili 2017 wenye lengo la kurahisisha huduma za usafiri na
usafirishaji nchini na nchi za jirani unaendelea kutekelezwa ambapo hivi karibuni kazi za ujenzi sehemu ya Isaka
– Mwanza yenye urefu wa kilometa 341unatarajiwa kuanza.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment