WAITARA AITAKA TRC KUTOA HUDUMA BORA
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (wa pili kushoto), akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo kikuu cha SGR Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa na kushoto ni Meneja Mradi Sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro, Mhandisi Simon Mbaga.
Serikali imelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha linatoa huduma bora na za viwango kwa Watanzania mara baada ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo mwishoni mwa mweziAgosti mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mwita Waitara, kufuatia wasiwasi wa wananchi kuhusu masuala ya miundombinu ya umeme wa reli hiyo ambapo pamoja na mambo mengine Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali kupitia Shirika hilo imejidhatiti kwa kuweka vyanzo vya umeme vitatu tofuati na vichwa vya kutumia dizeli ili kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza.
“Napenda kuwatoa wasiwasi Watanzania kuwa Serikali kupitia TRC imejipanga sawasawa kuhakikisha umeme hautakuwa changamoto wakati wa uendeshaji wa treni hii” amesisitiza Naibu Waziri.
Aidha, Waitara amelitaka Shirika hilo kujipanga na kuhakikisha kuwa wataalam wazawa waliopata ujuzi kwenye mradi huo wanatumika ipasavyo mara baada ya mradi kukamilika.
Waitara, amelipongeza Shirika hilo kwa kuajiri watalaam na kusimamia vizuri mradi huo kwa Sehemu ya Makutupora hadi Morogoro na Morogoro hadi Dar es Salaam.
Naibu Waziri Waitara amemhakikishia Mkurugenzi wa TRC kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa fedha ili mradi uweze kukamilika na Watanzania wafaidi matunda ya Serikali yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa, amesema kuwa TRC imeshaajiri wahandisi zaidi ya 200 ambao kwa sasa wamewekwa kwenye miradi ili kupata ujuzi na uendeshaji wa reli hiyo ya kisasa mradi utakapokamilika.
Kuhusu upatikanaji wa mabehewa Kadogosa amefafanua kuwa tayari manunuzi yako kwenye hatua nzuri na vichwa vitawasili mapema mwezi Julai na majaribio ya treni ya kwanza kwa sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro yatafanyika mwezi Agosti.
Naye, Meneja Mradi wa sehemu ya Morogoro - Dar es Salaam, Mhandisi Simon Mmbaga, amesema mradi huo kwa sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro umeshakamilika na asilimia zaidi ya 93 na kazi zinazoendelea kukamilishwa ni pamoja na kuunganisha mifumo mbalimbali katika vituo.
Naibu Waziri
wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amekamilisha ziara yake ya siku mbili ambapo
amekagua maendeleo ya ujenzi wa reli ya Kisasa ya SGR kwa sehemu ya Makutupora hadi
Morogoro na Morogoro hadi Dar esSalaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment