MICHEZO YA MEI MOSI 2021 IKULU YATINGA NUSU FAINALI NETIBOLI
1. Wachezaji Deta Petro
(GD) na Melania Magway (GK) wa timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini
(TPDC) wakiwahi mpira huku mfungaji Neema Mwanu (GS) wa Uchukuzi akijaribu kuupoka
katika mchezo wa netiboli wa Kombe la Mei Mosi uliofanyika
jana kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ambapo Uchukuzi walishinda kwa
magoli 36-25.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MABINGWA watetezi wa mchezo
wa netiboli, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu imetinga kwa kishindo hatua ya nusu fainali
kwa kuwa timu pekee iliyoshinda michezo yake yote minne kwa makundi yote mawili
ya michezo ya michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika kwenye uwanja wa CCM
Kirumba jijini hapa.
Mbali na pointi hizo
pia Ikulu imemaliza ikiwa na magoli mengi 166 ya kufunga; ambapo wamefuatiwa na
Uchukuzi wenye pointi sita na magoli 124 ikiwa nayo imeingia hatua ya nusu fainali
wote wakiwa kwenye kundi A; wakati timu za kundi B zilizofuzu hatua hiyo ni Wizara
ya Mambo ya Ndani ikiwa na pointi sita na magoli 128 wakifuatiwa na Tanesco yenye
pointi nne na magoli 118.
Kutokana na matokeo hayo
sasa Ikulu itakutana na Tanesco; huku Mambo ya Ndani watacheza na Uchukuzi katika
hatua hiyo itakayofanyika tarehe 27 April, 2021.
Kwa upande wa soka timu
za Tanesco na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wametinga hatua hiyo wakimaliza
kundi A wakiwa wote wana pointi tisa, lakini wanatofautiana katika magoli ya kufungwa
pekee; huku kundi B zimefuzu timu za Uchukuzi na TPDC wote wakiwa na pointi 10
lakini wanazidiana katika magoli ya kufunga na kufungwa.
Katika michezo iliyochezwa
jana kwa upande wa soka NCAA waliwafunga MWAUWASA magoli 19-0 yaliyofungwa na
Emmanuel Kabanyama manne; huku Regan Peter na Tumainiel Sandemu kila mmoja alifunga
magoli matatu, nao Liberatus Rwechungura, Detrum Mwakyalaba na Brown David kila
mmoja alifunga magoli mawili, pia Vicent Ngowo, Jacob Pangana Aidan Frank walifunga
goli moja kila mmoja.
Nayo Tanesco walifungwa
na RAS Mwanza kwa magoli 3-2. Magoli ya RAS yalifungwa na Fuma Kapeji mawili na
Peter Mumbar goli moja, na ya Tanesco yamefungwa na Ibrahim Said na Kurwa Mangara.
Katika michezo iliyofanyika
uwanja wa Nyamagana, Uchukuzi iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwafunga Mwanza
Jiji kwa magoli 4-0, yaliyofungwa na Joseph Paul, Rahim Ayesh, Mrisho Harambe na
Idrisa Bahatisha. Nao TPDC waliwashinda Wizara ya Kilimo kwa magoli 2-0
yaliyofungwa na Barnabas Mwashambwa na Daruweshi Shija.
Katika netiboli timu ya
Uchukuzi iliwashinda TPDC kwa magoli 36-25. Hadi mapumziko washindi walikuwa na
magoli 20-0; nayo Wizara ya Mambo ya Nje iliwafunga MWAUWASA kwa magoli 16-6,
yaliyofungwa na Patricia Kiswaga 12 na Jureck Mbise manne, wakati Salome
Emmanuel na Neema Maleko kila mmoja alifunga sita kwa MWAUWASA.
Michezo ya kuvuta
Kamba wanaume NCAA waliwashinda Wizara ya Habari (2-0); huku Chuo cha Mipango na
Wizara ya Kilimo walitoka sare ya 1-1; Tanesco walipata ushindi wa chee dhidi ya
PSSSF; nayo Habari walishindwa mbele ya Ukaguzi(2-0) na Mipango waliwavuta Nje
(2-0); wakati kwa upande wa wanawake Taasisi
ya Saratani Ocean Road waliwashinda Tanesco (2-0); TPDC waliwavuta NCAA (2-0);
Wizara ya Habari waliwavuta MWAUWASA (2-0); TPDC wakawashinda Habari (2-0) na Tanesco
wakapoteza tena kwa Mipango (2-0).
Michuano hiyo itaendelea
kesho kwa michezo ya mbio za kilometa 15 kwa wanaume na kilometa nane kwa
wanawake zitakazoanzia Igoma Stendi ya Magu hadi Sabasaba; pia kutakuwa na michezo
ya bao, karata na draft.

Post a Comment