CHAMURIHO AVITAKA VYAMA VYA MAKANDARASI NCHINI KUUNGANA
Makandarasi walioshiriki Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta
ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB),
wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho
(hayupo pichani) wakati akifunga mkutano huo jijini Mbeya.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amevitaka vyama vya makandarasi nchini kuungana ili kuwa na sauti moja itakayowarahisishia kuwasilisha maoni na matakwa yao kwa Serikali.
Hayo ameyasema Waziri huyo jijini Mbeya, wakati akifunga
Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021,
uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na kusisitiza kuwa kuungana
kwao kutaongeza weledi na uwezo wa rasilimali watu na fedha kwa makandarasi hao
na hivyo kuweza kupata kazi mbalimbali.
“Nimeona katika kandarasi kubwa changamoto iliyopo ni
kushindwa kupata kazi kwa sababu ya kutokidhi mahitaji ya zabuni, hivyo naomba mjitathmini
namna ya kuungana ili kuongeza weledi, hatimaye nanyi mpate hizi zabuni kubwa”,
amesema Chamuriho.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana
na Bodi hiyo katika kuhakikisha jitihada za kuwasaidia makandarasi wa ndani zinafanikiwa
na kufafanua kuwa katika Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 ilitenga
miradi maalumu mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambayo ilitekelezwa
na wakandarasi wazawa.
Mfano wa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Barabara
ya Urambo- Kaliua (Km 28) ambapo kwa sasa ujenzi wake umekamilika na Ludewa –
Kilosa (Km 24) ambao unaendelea kutekelezwa.
Amewaasa Makandarasi kuchangamkia fursa na kushiriki
ipasavyo pindi wanapopata zabuni ya kutekeleza miradi kwa kuifanya kwa ubora, kukamilisha
kwa wakati na kwa gharama iliyopangwa.
Kwa upande wake, Msajili wa CRB, Reuben Nkori,
ametaja changamoto zinazowakabili Makandarasi nchini kuwa ni pamoja na ukosefu wa
mitambo, ukosefu wa mitaji, uwezo mdogo katika kusimamia miradi ya ujenzi na uwezo
mdogo katika kusimamia rasilimali watu na rasilimali fedha.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Consolata Ngimbwa
amesema kuwa Bodi imeboresha Mfuko wa kusaidia Makandarasi na kuweza kutoa huduma
kwa Makandarasi wote wa ndani bila kujali daraja la ushitiri, ambapo kwa sasa unatoa
dhamana kuanzia shilingi milioni 100 badala ya shilingi milioni 50 ambazo zilikuwa
zikitolewa awali.
Mkutano huo uliobeba Kauli mbiu inayosema kuwa‘
'Juhudi za makusudi
za wadau, kuwezesha ukuaji wa makandarasi wa ndani’,ni wa kwanza kati ya mikutano
minne kwa mwaka huu, ambapo mingine inatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Dar
es Salaam, Arusha na Mwanza.
Imetolewa
naKitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment