KIWANJA CHA NDEGE MUSOMA KUGHARIMU ZAIDI YA BILIONI 30


Sehemu ya Watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wakimsikilizaNaibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (hayupo pichani) alipokutana nao katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya M/S Beijing Construction Engineering Group Company Limited kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma.

Mradi huo utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 30 unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 20 utahusisha barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege na jengo la zima moto.

Akizungumza mara baada ya kukagua kiwanja hicho mkoani Mara, Naibu Waziri Waitara amesema kukamilika kwa kiwanja hicho kutapandisha uchumi wa mkoa na kukuza utalii katika ukanda huo.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa uchumi wa Kanda ya Ziwa kwani kiwanja hiki kitapunguza gharama kubwa wanazotumia wananchi wa mkoa huu kwa kulazimika kutumia kiwanja cha Mwanza na badae kuingia kwenye magari kuja Musoma na Wilaya nyingine za Mkoa” amesema Naibu Waziri Waitara. 

Naibu Waziri Waitara ameutaka Wakala wa Barabarani Nchini (TANROADS) kuhakikisha unasimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyokubalika kulingana na mkataba.

Naye Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Musoma Mohammed Makau amesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo kutaruhusu ndege aina ATR 42 na Dash 8 Q 400.

Katika Hatua nyingine Naibu Waziri Waitara amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja linalounganisha mtaa wa Mwangaza na Msati, lililopo wilayani Tarime lililokatika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini  na kuridhishwa na ujenzi wake.

“Nawapongeza sana TANROADS hasa Meneja wa Mara maana siku limekatika nilipigiwa simu na mimi nikawasiliana na nyinyi na hapohapo na nimeelewa kuwa mnafanya kazi usiku na mchana, hongereni sana’ Amesema Naibu Waziri Waitara.

Naye Meneja wa TANROADS Mara, Mhandisi Felix Ngaile amesema kazi hiyo itakamilka kabla ya jumatatu na  magari yataruhusiwa kuanza kupita ili kuwarahisishia wananchi huduma za usafirishaji kutoka eneo moja kwenda jingine.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo  amezungumza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya WIzara hiyo na kuwataka kuongeza bidii kazini kwani Serikali haitavumilia mtumishi atakayeshindwa kutimiza majukumu yake kwa sababu ya uzembe.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara amekamilisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara kwa kukagua miundombinu ya uchukuzi.

 

(Imetolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini)

 

No comments