Sheikh Ponda ajiunga na ACT – Wazalendo, akabidhiwa kadi ya heshima ya Maalim Seif

 


Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania ,Sheikh Ponda Issa Ponda ametangaza kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo huku akikabidhiwa rasmi kadi ya heshima ya Maalim Seif ya Chama hicho.

Sheikh Ponda amesisitiza kuchangia nguvu katika Operesheni ya ACT Wazalendo ya Linda Demokrasia, inayolenga kurejesha haki, uwazi, na usawa katika michakato ya uchaguzi nchini Tanzania.

Sheikh Ponda amekabidhiwa Kadi hiyo leo Jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu mbele ya viongozi wengine waandamizi wa Chama hicho pamoja na Ngome zake.

Mbali na Kadi hiyo pia amekabidhiwa Katiba ya Chama hicho kama kitendea kazi chake katika harakati zake za siasa ndani ya Chama.

Akizungumza Mara baada ya kukabidhiwa vitu hivyo, Sheikh Ponda ametoa wito kwa vijana, wanawake, wazee, na viongozi wa dini,kuungana katika uwanja wa mapambano ya kudai haki mbalimbali zikiwemo za kisiasa kama vile kuhakikisha kura zao zinahesabiwa kwa haki na viongozi wanaochaguliwa wanawakilisha matakwa ya wananchi.

“Ndugu zangu mimi naamini amani ya kweli haiwezi kustawi pale ambapo kura zinaibiwa, sauti za wananchi zinakandamizwa, na sheria zinatumika kuwanyamazisha wale wanaosema ukweli.

Taifa letu linastahili kuongozwa kwa misingi ya sheria, ambapo kila mtu bila kujali cheo chake, dini yake, au kabila lake yuko chini ya sheria. Sheria inapaswa kuwa kinga ya haki za binadamu, si chombo cha kuwatesa wananchi,” amesema Sheikh Ponda.

Credit: Bongo5

No comments