Raia wa nchi 12 marufuku kuingia Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini tangazo la kupiga marufuku kusafiri kwenda nchini humo dhidi ya raia wanaotoka nchi 12, akitaja hatari za usalama wa kitaifa, kulingana na Ikulu ya White House.
Nchi hizo ni Afghanistan, Myanmar, Chad, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Equatorial Guinea, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen.
Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu, tarehe 9 Juni.
Hatua hiyo ya Trump imepingwa na mataifa yaliyoathiriwa.
Venezuela ni mojawapo ya nchi saba zilizoathiriwa na vikwazo vya sehemu.
Waziri wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello ameonya kuwa "kuwa nchini Marekani ni hatari kubwa kwa mtu yeyote, si kwa raia wa Venezuela pekee".
"Watu wanaotawala Marekani ni watu wabaya - ni mafashisti, ni watu wa itikadi kali ambao wanadhani wanamiliki dunia na kuwatesa watu wetu bila sababu", aliongeza.
Wakati huo huo, Somalia - ambayo sasa raia wake wapigwa marufuku kusafiri - imejibu kwa kuahidi mara moja kufanya kazi na Marekani kushughulikia masuala ya usalama.
Katika taarifa, balozi wa Somalia nchini Marekani, Dahir Hassan Abdi, anasema nchi yake "inathamini uhusiano wake wa muda mrefu" na Marekani.

Post a Comment