CCM yapitisha marekebisho matatu

 


Chama Cha Mapinduzi kimepitisha marekebisho matatu kwenye katiba yao.
Marekebisho hayo yaliyopitishwa ni pamoja na:

1. Mikutano ya CCM kwenye ngazi ya Sektratrieti ya Wilaya, kamati ya siasa Wilaya, Sekretariati ya mkoa, Kamati ya Siasa mkoa, Sekretariati ya kamati maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kamati maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mkutano Mkuu wa taifa vitakuwa vinafanyika kwa njia ya mtandao.

Kwenye pendekezo hilo, mikutano hiyo ya mitandao itafanyika kwa dharura tu na kwamba Katibu Mkuu wa chama atatakiwa kupewa taarifa pindi mikutano hiyo itakapokuwa inafanyika

2. Baraza la Wadhamini CCM litaongezeka kutoka kuwa na wadhamini 8 kwenda hadi wadhamini 9.

3. Baraza la wadhamini CCM litatoa idhini kwa maandishi kuhusu miradi ya CCM ambayo kamati za siasa na matawi mengine ya chama za CCM itakuwa zinataka kuanzisha au kutekeleza. Zamani mchakato huo ulikuwa unafanyika bila ulazima wa kuwepo kwa maandishi kutoka kwenye baraza la wadhamini.

Hii inamaanisha kwamba, kwa sasa Baraza hilo la wadhamini litakuwa linaombwa idhini kwa maandishi na oganaizesheni nyingine za CCM ili miradi iweze kutekelezwa na baraza hilo pia litatoa majibu kwa maandishi kwa wote watakaoomba idhini

UCHAGUZI MKUU 2025 KWA ILANI MPYA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliuambia mkutano huo;

"Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu, mtakumbuka kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa tarehe 18- 19 Januari 2025 ulipokea taarifa ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa, kuhusu utekelezaji wa kazi za chama na jumuiya zake kwa kipindi cha miaka miwili, 2022- 2024.

Lakini vile vile tulipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa kipindi cha miaka minne- mpaka mwaka jana uliofanywa na serikali zetu mbili, tulifanya marekebisho madogo ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 na likawa toleo la 2025 na kumchagua Makamu Mwenyekiti wa CCM bara.

Vile vile mkutano ule kwa kuzingatia ibara ya 100 (2) na 101(5b) za Katiba ya CCM ya mwaka 1977 ulimaliza kazi ya kuteua mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza. Aidha ulimthibitisha mgombea wa Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi baada ya kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM"

"Mkutano Mkuu huu ni sehemu muhimu ya maandalizi muhimu ya chama chetu kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025, kama inavyoonekana kwenye ratiba ya mkutano huu, ajenda kuu tutakayojadili kuanzia leo: kuangalia yaliyomo kwenye ilani tunayokwenda kuinadi kwa wananchi katika uchaguzi ujao.

 Itakumbukwa kuwa katika kutimiza jukumu lake la kikatiba lililoanishwa chini ya Ibara ya 103 (4) ya Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya CCM taifa katika kikao chake kilichofanyika Dodoma tarehe 10 Machi mwaka huu pamoja na mambo mengine ilipokea na kuthibitisha ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka huu, hivyo basi kesho tutafanya uzinduzi wa Ilani tutakayokwenda kuinadi kwa wananchi ili watupe imani na ridhaa ya kuturudisha kuendelea serikalini katika kipindi kingine cha miaka mitano"


No comments