SAFARI YA MKESHA WA MAZISHI YA MALU STONCH KUANZIA KIDULI GARDEN

 

Wanamuziki wa FM Academia na baadhi ya wadau wa muziki, leo jioni watakutana New Kiduli Garden kabla ya kuelekea kwenye mkesha wa mazishi ya Malu Stonch.
Hapo Kiduli Garden, Magomeni Kanisani, kutakuwa na chakula cha usiku kisha baadae safari ya kuelelea msibani Salasala itaanza.
Meneja wa Kiduli Garden, Lugano Matola ameiambia Saluti5 kuwa watagharamia chakula hicho cha usiku baada ya kupata baraka za FM Academia.
"Tutakuwa pamoja na wanamuzki wote wa FM Academia na wadau wa muziki, tutapata chakula cha pamoja kabla ya kuelekea msibani, tutaandaa pia usafiri kwa wale ambao watakuwa hawana vyombo vyao binafsi vya usafiri," ameeleza Lugano.
Meneja huyo wa Kiduli akaongeza: "Kwa kuwa wanamuziki wanakwenda kukesha msibani, tumeona ni vema tuwaalike waje wapate chakula cha usiku.
"Tumeishi vizuri na FM Academia, Malu Stonch alikuwa rafiki ya kila mtu hapa Kiduli, tumeona hii ni moja ya njia za kuwafariji ndugu zetu.
"Na pia tutatumia nafasi hiyo kukabidhi mchango wa mazishi ya Malu Stonch kutoka kwa Kiduli Garden na wadau wao.
"Kama kuna makundi mengine yaliyokuwa yanaendesha michango, basi tunawakaribisha ili tukabidhi pamoja na iweze kuwasilishwa msibani."
Malu Stonch atazikwa kesho Jumamosi katika makaburi ya Kwa Kondo Ununio.
Ratiba inayonyesha shughuli mbali mbali ikiwemo Misa, zitafanyika nyumbani kwa marehemu kuanzia saa 2.30 asubuhi.

Said Mdoe
12/4/2024

No comments