Yanga: Mzunguko bure mechi ya Mamelodi

 

Kuelekea mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, miamba ya soka nchini, Yanga, imetangaza kuwa mashabiki watakaokaa mzunguko wataingia bure.

Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema katika maeneo mengine ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, mashabiki watalipia. Watakaokaa VIP A watanunua tiketi kwa shilingi 30,000, wale wa VIP B watatoa 20,000 na katika VIP C watapata burudani ya buku teni tu.

Kuhusu hali ya kiungo wao tegemezi, Pacome Zouazoua ambaye alipata majeraha katika mechi iliyopoteza dhidi ya Azam, hali yake bado haijakaa sawa, akifafanua kuwa madaktari wa timu ya taifa ya Ivory Coast, ambao wamemuita kambini Ufaransa, wamemuomba huko ili waone nini wanaweza kumsaidia.

Alisema madaktari hao watawataarifu kuhusu hilo na wao kama klabu watatoa taarifa. Aidha, mlinzi Yao Kouassi aliyepata majeraha pia katika mechi hiyo hali yake bado ni hamsini kwa hamsini wakati Daktari wa Boli, Khalid Aucho yeye anaendelea kuimarika na beki wao Kibwana Shomari anaripotiwa kuwa ataanza mazoezi Jumatatu ijayo.

No comments