Serikali yadhamiria kuimarisha Uwanja wa Ndege Julius Nyerere
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imekusudia kuuimarisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo mkoani Dar es Salaam, ili uwe kitovu cha usafiri wa anga kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema ili kufanikisha jambo hilo Serikali imepanga kuufanyia ukarabati uwanja namba mbili (terminal 2) uliopo JNIA.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing B 737-9 Max iliyowasili nchini ikitokea Seattle, Marekani, Majaliwa amesema uwanja wa ndege namba mbili wa JNIA utakapokamilika utakuwa mahususi kwa ndege zinazofanya safari zake ndani ya Tanzania.
Amesema uwanja huo namba mbili utasaidia kuongeza miruko ya ndege na safari hasa za kwenda katika masoko mbalimbali.
Waziri Mkuu ameziagiza taasisi zote zinazotoa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuboresha huduma zao li kuvutia wateja na kuufanya uwanja huo kutoa huduma bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Post a Comment