Mwandishi aliyehukumiwa kifungo DRC aachiwa huru

 


Mwanahabari mashuhuri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameondoka katika jela maarufu ya Makala katika mji mkuu Kinshasa licha ya jaribio la mamlaka kuzuia kuachiliwa kwake.

Stanis Bujakera alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani siku ya Jumatatu kwa kueneza habari za uongo, lakini tayari alikuwa ametumikia muda huo katika kizuizi cha kabla ya kesi.

Waendesha mashtaka wa serikali walikata rufaa wakidai kuwa hukumu hiyo ni ndogo lakini baada ya kuchelewa kwa saa kadhaa, Bw Bujakera aliachiliwa.

Waendesha mashtaka walikuwa wameomba Bw Bujakera afungwe jela miaka 20.

Mashirika ya haki za kibinadamu yalitaja kukamatwa kwake kuwa ni shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.

Alishtakiwa kwa kuandika makala katika jarida la lugha ya Kifaransa la Jeune Afrique mnamo Julai, ambayo ilidai kuwa wanajeshi walihusika katika mauaji ya mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Cherubin Okende.

Nakala hiyo haikutiwa saini na haikubeba maandishi ya Bw Bujakera.

Bw Okende, waziri wa zamani na msemaji wa chama cha upinzani cha Ensemble Pour la Republique (United for the Republic), alitoweka Julai mwaka jana.

Mwili wake uliokuwa na risasi ulipatikana baadaye kwenye gari lake mjini Kinshasa.

bbc

No comments