Mkurugenzi Kasulu Mji atoa maagizo matano muhimu kwa Watendaji Kata



Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Mji Kasulu, Mheshimiwa Vumilia Simbeye ametoa maagizo matano muhimu kwa watendaji wa kata za halmashauri hiyo wakati wa kikao chake kilichofanyika leo.

Kabla ya kutoa maagizo hayo, Mkurugenzi Simbeye alianza kwa kwa kumshukuru kwa dhati Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuona, kumuamini, kumteua na kumuunganisha na timu hiyo ili aweze kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi wa Kasulu mjini kwa kuwaletea maendeleo endelevu.


Simbeye aliwahimiza watendaji hao kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta tija kwa wananchi wa Kasulu na Tanzania kwa ujumla, Kupandisha mapato kwa kubaini vyanzo ambavyo vipo na havijasajiliwa sambamba na kubuni vyanzo vipya huku wakiziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Halmashauri.

Aidha, Mkurugenzi Simbeye aliwataka watendaji hao kusimamia vizuri miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati sambamba na kukagua ubora wake kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali. 


Pia, kiongozi huyo aliyeteuliwa hivi karibuni alikemea vikali tatizo la rushwa holela kwa tarafa zote mbili zenye kata 15 na mitaa 108 ya Halmashauri hiyo, huku akiahidi katua kali za kisheria kuchukuliwa kwa watendaji wote watakaobainika kujihusisha na rushwa.

Mwisho aliwaelekeza watendaji wa Kata kwa kushirikiana na wasaidizi wao kuhakikisha wanaondoa kabisa malalamiko mbalimbali ya wananchi katika maeneo yao. Na ili kuhakikisha kazi zote katika Halmashauri hiyo zinakwenda vizuri, amewaruhusu watendaji hao kumfikia wakati wowote katika utekelezaji wa majukumu yao kabla mambo hayajaharibika kwenye maeneo yao. 


No comments