Mfahamu Simbeye, Mteule wa Rais Samia anayeamini uwezo wa vijana na busara za wazee

 


Na Ojuku Abraham
UMBALI wa Kilometa 735 kutoka Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma, katika Kata ya Tunduma, iliyopo mpakani mwa nchi ya Zambia, mkoani Songwe, alizaliwa kijana ambaye leo ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Akiwa na umri wa miaka 45 sasa, Mkurugenzi huyo mpya ni miongoni mwa vijana kadhaa ambao wameendelea kuaminiwa na serikali kushika nafasi mbalimbali za kisiasa, kiutendaji na kijamii na hivyo kuifanya nchi kuwa na mawazo mapya ya namna ya kuendeleza.

Baada ya kizazi cha wapigania Uhuru chini ya Mwalimu Julius Nyerere, na baadaye kupokewa na vijana wao, Benjamin William Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete, John Pombe Magufuli na sasa Samia Suluhu Hassan, mama anawapa majukumu vijana wadogo zaidi ambao wanawakilisha kizazi chao kipya cha uongozi.

Kiongozi huyu ana vitu vingi kichwani mwake ambavyo endapo atavifanyia kazi kwa upande wake na ushauri wake ukachukuliwa na wengine, hakuna shaka kuna matokeo chanya. Ojuku Blog ilimtafuta na kufanya naye mahojiano mafupi kama ifuatavyo:

 

Swali: Vumilia Simbeye ni nani na historia yake kwa ufupi

 

Kuzaliwa:

Kwa majina naitwa Mwalimu VUMILIA JULIUS SIMBEYE, mzaliwa wa Tunduma mkoani Songwe. Nilizaliwa miaka 45 iliyopita katika Kata ya Tunduma, Tarafa ya Tunduma mkoa wa Songwe.

Ni mtoto wa pili kuzaliwa kwa mzee Julius Moses Simbeye baba yangu baada ya kaka yangu na ni wa pili pia kwa mama yangu Betina Andongolile Mwakipesile mama yangu baada ya dada yangu. Ambapo, kwa bahati mbaya, baba yangu mzazi alifariki tarehe 24/8/2004 na mama alifariki tarehe 1/9/2015. Wote walizikwa Tunduma, wilayani Momba mkoani Songwe. Bwana alitoa na Bwana ametwaa; jina lake lihimidiwe.

Elimu:

Nilianza elimu yangu ya msingi mwaka 1988 katika Shule ya Msingi Maporomoko Tunduma. Nilijiunga na elimu ya Sekondari mwaka 1995 na kuhitimu kidato cha 4 mwaka 1998 katika Shule ya Sekondari Irambo Mbeya vijijini. Mwaka 1999 nilijiunga na Shule ya Sekondari Malangali Iringa kwa ajili ya masomo ya Kidato cha 5 na 6 baada ya kufaulu Kidato cha 4 na kuhitimu Kidato cha Sita mwaka 2001. Baadae mnamo mwaka 2004 nilijiunga na Stashahada (Diploma) ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Morogoro na kuhitimu mwaka 2006. Hatimaye mwaka 2010 nilijiunga na Shahada ya kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha RUCU mjini Iringa na kuhitimu mwaka 2013. Hatimaye mwaka 2018 nikajiunga na Shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Mzumbe cha Morogoro na kuhitimu mwaka 2020.

Ajira:

Niliajiriwa mwaka 2006 wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma kama mwalimu wa Shule ya Sekondari. Mwaka 2008 nilihamishiwa katika Shule ya Sekondari Mafiga iliyopo katika Kata ya Mafiga, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro.

Mwaka 2015 nilibadidilishiwa majukumu na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro na kuwa Afisa Elimu Taaluma Msaidizi; hadi mwaka 2021 nilipoteuliwa rasmi kuwa Afisa Elimu Taaluma Sekondari, Halmashauri ya Mji Ifakara. Tarehe 9 Machi, 2024 nilipata bahati ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu hadi sasa.

 

Swali: Umetoka kuwa Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Ifakara na kuwa Mkurugenzi. Unafikiri ni hatua muafaka au umepiga hatua kubwa kwa haraka?

Nimepiga hatua kubwa kwa haraka lakini, naamini kwamba; ni hatua muafaka kwa mimi kuwatumikia watanzania wenzangu katika eneo nililo aminiwa. Kwani; uongozi ni ushirikiano mzuri baina ya wale walio chini yangu na wananchi ambao ndio kitovu cha nafasi niliyokabidhiwa. Aidha, uongozi ni kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yatolewayo na serikali. Lakini kubwa zaidi, uzalendo ndio nguzo ya maendeleo. Na hivyo vyote ni sehemu ya maisha yangu ya uongozi tangu enzi na enzi.


Swali: Umekwenda kuongoza moja ya maeneo yanayopigiwa kelele kama vyanzo vya upigaji fedha za serikali. Nini mtazamo wako?

Kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni zinafuatwa katika kufanya matumizi ya fedha za serikali zinazoletwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu.

(i) Kusimamia na kuhakikisha kwamba; miradi ya maendeleo inakamilika ndani ya muda uliopangwa na inatelelezwa kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotolewa.

(iii) Kuwapa maelekezo mahsusi wakuu wote wa Idara na vitengo juu ya kuwa makini na na matumizi ya fedha za Serikali sambamba na kuwapa angalizo ili wasije kuwa sehemu ya Halmashauri kuendelea kunuka harufu mbaya za upigaji.

(iv) Kushirikiana na vyombo katika kuwachukulia hatua wale wote wataobainika ama wataoonesha dalili za kutaka kupiga fedha zinazotolewa Serikali.    

 

Swali: Kutokana na kuwa kwako mtumishi wa serikali, bila shaka unafahamu changamoto wanakutana nazo ambazo wewe kama Mkurugenzi utazifanya kuwa kipaumbele. Ni zipi changamoto za muhimu?

 

(i) Madai ya malimbikizo ya mishahara.

 

Suluhu; nitaboresha mawasiliano na mamlaka husika kukumbushia juu ya madai ya watumishi wangu.

(ii) Madai ya fedha za likizo, kustaafu na za uhamisho.

Suluhu; nitahakikisha kila Idara inakuwa na kanzidata, mikakati na ushauri wa namna bora ya kupunguza kama siyo kuondoa kabisa manung'uniko ya watumishi mahala pa kazi.

(iii) Mikopo ya Hazina kukopeshwa kwa wakuu wa Idara, wanaokaribia kustaafu na wenye mishahara mikubwa wakati kuna waliopo huko chini wanakosa kabisa mikopo.

Suluhu; watumishi wa chini na wenye mishahara midogo nitawapa kipaumbele.

(iv) Mgawanyiko wa watumishi kwenye Idara za ndani ya Halmashauri; wakuu wa idara kufanya kazi na mtu mmoja au wawili wa kwenye idara yake na kuwaona wengine kama siyo kitu.

Suluhu; nitawaunganisha wakuu wa idara na walio chini yao ili wote wafanye kazi kwa umoja na ufanisi mkubwa. Kwani; umoja na mshikamano ni nguzo kwa ushindi wenye tija.

(v) Watumishi kukata tamaa kutokana na lugha kali na majibu mabovu ya baadhi ya maafisa waandamizi.

Suluhu; nitawapa msimamo wangu kwa kuwataka maafisa kutoa huduma kwa watu kwa kutumia lugha nzuri na bila upendeleo kulingana na maadili ya utumishi wa umma.

Vumilia Simbeye akiwa katika moja ya majukumu yake ofisini


Swali: Hiyo nafasi ni ya kuteuliwa. Je, umewahi kuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa?

Siasa ni maisha na maisha ni siasa. So, mimi ni muumini wa kuchochea siasa safi zenye tija kwa maendeleo ya wananchi na taifa letu. Na uongozi ni uongozi; waweza kuwa wa kuteuliwa au wa kuchaguliwa. Nami kama Kiongozi, naweza kuwa wa pande zote kwa sababu uongozi ni matokeo chanya na matokeo chanya ni maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Swali: Wewe bado ni kijana. Unafikiri ni wakati sasa wa nafasi muhimu na nyeti kama yako kuanza kushikiliwa na vijana au iende kwa awamu na kwa nini?

Kimsingi huu ni wakati sahihi wa vijana kushika nafasi nyeti kama yangu lakini kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya Serikali pamoja na hekima, busara na baraka za wazee. Kwani, utu uzima ni dawa …

Swali: Nini ndoto yako kama kiongozi mchanga mwenye malengo makubwa?

 Ndoto yangu kubwa kama Kiongozi mchanga lakini mwenye uwezo mkubwa na kama mzalendo wa kweli ni kuhakikisha naacha alama kwa kuwa sehemu ya ushindi wa taifa letu la Tanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Swali: Nini wito wako kwa vijana, hasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu?

 

Tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025; napenda kutoa wito kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 18 kujiandikisha kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura ili waitumie haki yao kikatika kwa kushiriki uchaguzi na kuwachagua viongozi watakaowaletea tija na maendeleo endelevu katika maeneo yao.

 

Swali: Taifa lina changamoto ya matumizi ya madawa ya kulevya, biashara ya ngono, rushwa na ukosefu wa maadili. Kwa mawazo yako, nini kifanyike ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto hizi?


(i) Elimu juu madhara ya dawa za kulevya, rushwa na biashara ya ngono kuendelea kutolewa.

(ii) Elimu ya Mikopo ya asilimia 10 ya vijana, wanawake na wenye ulemavu iendelee kutolewa kwa waathirika hao ili waone umuhimu na faida ya kujishughulisha na kujiingizia kipato badala ya kupoteza muda kwa kukiuka maadili.

(iii) Kujenga vituo maalumu vya kuwashauri na kuwanasihi waathirika hao kwa kuwapelekea washauri na wawezeshaji watakaowarejesha kwenye hali zao halisia.

(iv) Kuunda Kamati za kubaini, kufichua na kuwachukulia hatua kali za kisheria wauzaji wa dawa za kulevya ili kuwanusuru vijana wasijiingize kwenye janga hilo.


Swali: Ukipata nafasi ya kushauri jambo, lipi ni la msingi kwa sasa ambalo ungetamani taifa lifanye?

(i) Katika kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 ningependa kuzishauri Halmashauri zote kupitia watendaji wa Kata na Mitaa pamoja na wenyeviti wa mitaa; kusoma mapato na matumizi kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika maeneo yao ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

(ii) Kwa maeneo yenye shughuli za Kilimo kama Kasulu Mji, maafisa Kilimo watembelee vijijini mara kwa mara ili kutoa elimu ya Kilimo chenye tija.

(iii) Elimu ya ulipaji na faida za ulipaji Kodi ya Serikali iendelee kutolewa na Maafisa Biashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kupandisha mapato ya Halmashauri nchini.

(iv) Uongozi shirikishi wa namna bora za kubuni vyanzo vipya vya mapato utumike ili ukusanyaji wa mapato uendane na miradi ya kutosha ya maendeleo kwa faida ya watanzania kwa ujumla wake.

(v) Motisha kwa watumishi wanaotekeleza majukumu yao vizuri na yanapimika. Hususani kwa walimu  ili kuongeza morali katika uwajibikaji.

(vi) Uboreshwaji wa miundombinu ya barabara hususani vijijini uendelee kufanyika ili kuleta nafuu kwa wakulima na wafanyabiashara kisafirisha mazao na bidhaa zingine kuelekea kwenye masoko.

Neno lolote kwa taifa

Kwa kuwa uzalendo wetu ndio utaifa wetu; basi ni vyema kila mtanzania akawa mzalendo kwa nchi yetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa na taifa imara lenye amani na utulivu daima.

No comments