Kwanini Marekani inasema 'uhai' wa Ukraine uko hatarini?

 

Siku ya Jumanne, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alijaribu kuwahakikishia washirika wake wa Ulaya kwamba utawala wa Rais Joe Biden unasalia na nia ya kuunga mkono Ukraine, ingawa Washington kwa sasa haina pesa za kusambaza silaha.

"Wanajeshi wa Ukraine wanakabiliwa na hali ngumu na mapigano makali. Raia wa Ukraine wanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora ya Urusi na droni za Iran.

Lakini Ukraine haitarudi nyuma, na hata Marekani haitarudi nyuma. Hivyo ujumbe wetu leo ni wa wazi; Marekani haitoiwacha Ukraine ishindwe. Muungano huu hautaruhusu Ukraine kushindwa, na ulimwengu huru hautaruhusu Ukraine kushindwa,” alisema Austin katika mkutano uliofanyika katika kambi ya kijeshi ya Ramstein nchini Ujerumani.

Lakini Austin hakufafanua ni kwa jinsi gani Washington inakusudia kuunga mkono Ukraine wakati Congress haina haraka kuidhinisha pesa kwa madhumuni hayo.

Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Austin aliwaambia waandishi wa habari: "Uhai wa Ukraine uko hatarini... Washirika wetu wanaendelea kuongeza juhudi zao, na Marekani lazima pia ifanye hivyo."

Maafisa wa Marekani wanakiri kwamba upungufu wa ufadhili tayari una athari kubwa kwa vita nchini Ukraine, kwani Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine vinapigana kwa zana chache na kuhifadhi risasi.

"Nadhani washirika wanafahamu sana hali ya ufadhili, na Waukraine wanaelewa hilo zaidi kuliko mtu mwingine yeyote kwa sababu ya uhaba (wa silaha na risasi) ambao umetokea kama matokeo ya sisi kutokuwa na uwezo wa kuwapatia silaha," afisa mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani aliambia Reuters kwa sharti la kutotajwa jina.

Wiki iliyopita, utawala wa Biden ulisema utatuma msaada wa kijeshi wa dola milioni 300 kwa Ukraine.

Maafisa wa Marekani hawaondoi uwezekano kwamba utawala wa Marekani utaweza kupata pesa, lakini kama wanavyosisitiza, fedha hizi hazitaweza kuziba pengo la muswada uliozuiwa na Congress ambao utatoa msaada kwa Ukraine kwa kiasi cha dola bilioni 60.

Siku ya Jumanne, Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky alihutubia nchi za muungano wa Nato kutoka Kyiv na kutoa ombi la kupewa mifumo ya ziada ya ulinzi wa anga. Kulingana na yeye, mwezi Machi pekee, wanajeshi wa Urusi walitumia makombora 130, na zaidi ya ndege zisizo na rubani 320 na karibu makombora 900 ya kuongozwa dhidi ya Ukraine.

Katika hali hii, licha ya uhakikisho wote wa Lloyd Austin, nchi za Ulaya zinazidi kujadili jinsi ya kujitegemea kijeshi.

"Inazidi kuwa vigumu kwa viongozi wa Marekani kusafiri hadi Ulaya wakiwa na hakikisho kwamba Marekani imejitolea kwa Ukraine kwa muda mrefu," Rachel Rizzo, kutoka kituo cha Atlantic Council of Europe Center, alinukuliwa na Reuters.

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel alisema hivi karibuni, bara hilo lazima lijenge upya uchumi wake, akisisitiza kwamba Ulaya haiwezi tena kutegemea mzunguko wa uchaguzi wa Marekani.

"Huu ni wakati wa mabadiliko ya kweli kuhusu usalama na ulinzi wetu. Kwa miongo kadhaa, Ulaya haijawekeza vya kutosha katika usalama na ulinzi wake. Sasa, tunapokabiliwa na tishio kubwa zaidi la usalama tangu Vita vya Pili vya Dunia, ni wakati wa kuchukua hatua kali na madhubuti kuwa tayari kujilinda na kuweka uchumi wa Umoja wa Ulaya kwenye msingi wa vita," Michel aliandika katika hotuba yake kwa wanachama wa Baraza la Ulaya.

Ukraine inahitaji silaha


Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, ambaye alishiriki katika mkutano wa Ujerumani, aliandika kwenye Facebook kufuatia mkutano huo kwamba washirika wa Magharibi waliamua kutuma makombora na mifumo ya ulinzi wa anga kwa jeshi la Ukraine.

Umerov alisema wakati wa mkutano huo, Ukraine ilitangaza mipango yake ya 2024, ilizungumza juu ya ujenzi wa ngome na kutaja mahitaji yake.

Kulingana na mkuu wa idara ya ulinzi ya Ukraine, washiriki wa mkutano huo walijikita kwenye usambazaji wa silaha.

"Silaha ni kitu ambacho mashujaa wetu wanahitaji sana. Hii ilikuwa mada kuu ya mkutano, "Umerov aliandika. "Washirika wametangaza msaada mpya wa silaha."

Nchi kadhaa zilizoshiriki katika mkutano huo zilikubali kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa silaha kwa Ukraine.

"Tunashukuru washirika wetu kwa kutafuta na kupata silaha duniani kote, ambazo ni muhimu sana kumfukuza mvamizi," anaandika Umerov.

bbc


No comments