ASHA BARAKA: HUWEZI KUPAMBANISHA BENDI MBILI KWA MALIPO YA UBWABWA

 


Mmiliki wa Twanga Pepeta, Asha Baraka amesema sio kweli kuwa alifanya vurugu na wala hakulalamika nyota ya bendi yake kuchafuliwa na FM Academia.
Aidha, Asha Baraka amesema alichofanya yeye ni kuushutumu uongozi wa Kiduli Garden kwa kuleta ujanja wa kuzipambanisha bendi mbili jukwaani kwa malipo ya ubwabwa.
Juzi usiku kwenye onyesho la Twanga Pepeta ndani ya Kiduli Garden Magomeni, FM Academia walipanda jukwaani kusalimia kisanii.
Baada ya onyesho inasemekana Asha Baraka alitinga ukumbini na kufanya kikao na wasanii wake pamoja na meneja wa Kiduli Garden.
Patcho Mwamba akalalamika kuwa Asha Baraka anahujumu dansi kwa kufanya fujo kisa tu FM Academia imepanda jukwaa la Twanga Pepeta.
Patcho aliiambia Saluti5 kuwa wao walialikwa chakula cha jioni hapo Kiduli na uongozi wa ukumbi huo kama walivyoalikwa pia wasanii wa Twanga Pepeta.
Baadae FM wakaombwa na uongozi wa Kiduli kupamba jukwaani kusalimia kisanii kwa nyimbo chache, hatua ambayo Patcho anadai waliikubali kwa lengo la kukuza undugu lakini likamchukiza Asha Baraka.
Patcho anasema hata wao FM Academia mwanzoni waligomea ombi hilo lakini baada ya kushawishiwa sana wakakubali.
Saluti5 ilipowasiliana na Asha Baraka ikapata upande wa pili wa sakata hilo.
Kwanza kabisa Asha Baraka anasema wakati anafika ukumbini shwo ilikuwa imemalizika na Patcho Mwamba hakuwepo, alishaondoka hivyo malalamiko yake ameyatoa kwa kusimuliwa.
Asha Baraka anaeleza hivi: "Wiki iliyopita Kiduli walinipigia simu wakitaka tufanye show ya pamoja ya vunja jungu sisi na FM Academia, nikapeleka wazo kwa wasanii, wakalipinga.
"Wasanii walisema show kubwa kama hiyo huwezi kuifanyika kwa matayarisho ya wiki moja, lakini pia wakadai Twanga kufanya show na FM ni biashara nzuri lakini isiyopaswa kurudiwa kila baada ya muda mfupi.
"Nikawaambia Kiduli onyesho hilo halipo, wakaingia makubaliano ya kufanya show ya Twanga Jumatatu.
"Jumatatu asubuhi wakanipigia na kusema wanawaalika wasanii wa Twanga kupata chakula cha jioni kabla ya onyesho, wakasema na FM Academia pia watakuwepo, nikawaambia sawa hakuna shida.
"Jioni saa 12 nikapita ukumbini nikakuta chakula kiko jikoni na wasanii bado hawajafika, boss wa Kiduli akanisisitizia tena kuwa FM Academia watakuwepo kwenye mwaliko wa chakula, nikamwambia sio FM tu hata akitaka kualika Dar es Salaam nzima afanye hivyo.
"Usiku wa manane nikiwa nyumbani kwangu Magomeni nikawa nasikia nyimbo za FM zinalia, nikampigia meneja wa bendi Martin Sospiter nikamuuliza FM wamepanda jukwaani akasema ndio, waliombwa na meneja wa Kiduli wawapishe kidogo FM, nikamwambia nakuja huko huko.
"Nikafika ukumbini wakati onyesho limeshamalizika hata wasanii wa FM sikuwaona, wa Twanga walibakia baadhi.
"Nikaitisha kikao na wasanii wangu pamoja na meneja wa Kiduli, nikasema bendi yetu imepigishwa show ya bendi mbili kinyemela kwa kudanganyiwa pilau nyama na ubwabwa.
"Ukweli ni kwamba tunapaswa kulinda brand za bendi zetu, Kiduli wametengeneza show ya bendi mbili kinyemela baada ya kuwagomea kufanya onyesho la pamoja.
"Ule mwaliko wa chakula cha jioni kumbe ilikuwa ndio janja yao, wamefanya kosa kubwa sana hata FM Academia wamekosea.
"Leo huwezi kumwalika Diamond, Ali Kiba au hata Isha Mashauzi kwenye harusi halafu ukawaambia waimbe, hawatakubali.
"Nalaani sana bendi mbili kupambanishwa jukwaani kwa mwaliko wa ubwabwa.
"Twanga Pepeta ni brand na FM Academia ni brand, unapotaka kuzikutanisha bendi hizi jukwaani kwa staili yoyote ile ni lazima uzilipe pesa ya maana."

Said Mdoe
13/3/2024

No comments