Rais Samia aalikwa Vatican na Papa Francis
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho anatarajia kufanya ziara ya Kikazi Vatican ambapo atakutana na Papa Francis I.
Ziara ya Rais Samia inatokana na mwaliko Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani ambao aliupokea.
Atakapowasili, atapokelewa rasmi na Papa Francis kwenye Ofisi za Papa na kufanya naye mazungumzo ya faragha, kisha Papa Francis atakutana na ujumbe mzima wa Rais Samia.
Kwa mujibu wa taarifa aliyotoa Waziri wa Mambo ya Nje, kupitia mtandao wake wa X, Januari Makamba amesema baada ya Mkutano na Papa Francis, Rais Samia atakutana na Kadinali Pietro Parolin, Msaidizi Mkuu wa Papa Francis kwenye Serikali ya Vatican pamoja na Askofu Paul Gallagher, Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa wa Vatican.
“Katika ujumbe wake, pamoja na viongozi wa Serikali na Wasaidizi wake,”amesema Makamba.
Amesema Rais Samia ataongozana na wawakilishi wa waumini Wakatoliki kukutana na Papa Francis ambao ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika, Eveline Ntenga.
Pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa, Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti wa Umoja Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania (VIWAWA), Leonard Mapolu.
Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Zanzibar, Bwana Dalmas Gregory, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Dar es Salaam, Teresia Seda.
Aidha ziara hiyo inafuatia mwaliko wa Baba Mtakatifu Francis kwa Rais Samia.

Post a Comment