Nani anataka kumuua Paul Makonda?

Hakuna ubishi kwamba Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Paul Makonda ana maadui ndani ya chama chake.

Na maadui hawa siyo watu wadogo, bali ni wazito wenye uwezo hata wa kuitoa roho yake.

Hauhitaji kuwa na akili kubwa kuweza kubaini ukweli huu, isipokuwa kwa kufuatilia tu ziara ya kiongozi huyu huko mikoani, kinachotokea katika mikutano yake, kinachosemwa na makada wenzake na mwishowe kinachotoka kinywani mwake.

Kubwa linaloogofya, ni kauli yake inayoashiria kwamba wapo watu, bila shaka ndani ya CCM ambao wanamroga, wanaweka sumu katika vyumba anavyolala, wakiwa na lengo la kumdhuru.

Nasema hawa maadui wapo ndani ya CCM kwa sababu siamini kama watu wa vyama vya upinzani wanaweza kupenya kuingia katika chumba anacholala Makonda, kwa kuwa hawajui atalala wapi, muda gani na wapi.

Zipo habari ambazo hazijathibitishwa kwamba leo akiwa Songwe, Makonda aliliacha jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya mkutano wake, akaenda kuzungumza na wananchi akiwa ndani ya gari lake.

Kuzungumzia kutoka ndani ya gari siyo jambo geni, lakini mazingira anayopitia hivi ssasa yanawafanya watu kuhusisha tukio hilo na kinachojiri.

Suala la kujiuliza, ni akina nani wana mpango wa kumpoteza Makonda? Kwa nini?

Pengine tunaweza kusema ni mbinu za kisiasa, sawa. Lakini haya ni madai mazito mno kuyachukulia kikawaida.

Makonda siyo mgeni serikalini wala chamani. Anapotoa madai kama haya, ni lazima ana ABC ya kinachoendelea.

Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vina wajibu wa kufanya kitu katika hili. 

No comments