Christopher Saunders: Askofu wa zamani wa Broome ashtakiwa kwa ubakaji nchini Australia
Askofu wa Australia Christopher Saunders ameshtakiwa kwa ubakaji na msururu wa makosa ya kihistoria ya ngono - mengine dhidi ya watoto.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 74 alikamatwa huko Broome siku ya Jumatano, kufuatia uchunguzi ulioamriwa na polisi wa Australia Magharibi Pamoja na Papa Francis.
Bw Saunders, ambaye alikana madai hayo hapo awali, alinyimwa dhamana na atafikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.
Yeye ni mmoja wa makasisi wakuu wa Kikatoliki kukabiliwa na mashtaka ya aina hii.
Bw Saunders anashtakiwa kwa makosa mawili ya ubakaji, makosa 14 ya shambulio lisilo halali na la aibu, na makosa matatu ya kushughulika na mtoto kwa njia isiyo ya heshima kama mtu mwenye mamlaka.
Anadaiwa kutekeleza makosa hayo katika miji ya mbali ya Australia Magharibi ya Broome, Kununurra na ile ya jamii ya Waaboriginal ya Kalumburu kati ya 2008 na 2014.
Kando na marehemu Kadinali George Pell, ambaye alifungwa jela na kisha kuachiliwa, Bw Saunders ndiye afisa mkuu wa Kanisa Katoliki nchini kushtakiwa kwa makosa ya ngono ya watoto.
Katika taarifa siku ya Alhamisi, Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki wa Australia liliahidi kushirikiana na polisi, na kusema mashtaka dhidi ya Bw Saunders ni "mazito sana na ya kuhuzunisha sana, hasa kwa wale wanaotoa madai hayo".
"Ni sawa na sahihi, na kwa kweli ni muhimu, kwamba madai yote kama haya yachunguzwe kwa kina," Askofu Mkuu wa Perth Timothy Costelloe alisema.
Akiwa ametawazwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1976, Bw Saunders ametumia muda mwingi wa kazi yake katika eneo la kijijini la Kimberley kaskazini-magharibi mwa taifa hilo, na aliteuliwa kuwa Askofu wa Broome mwaka wa 1996.
Dayosisi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 770,000 (maili za mraba 297,000) - eneo ambalo lina ukubwa wa Uturuki - na linajumuisha baadhi ya maeneo ya mbali zaidi ya nchi.
Anajulikana sana kwa kushirikiana, katika kazi yake ya utetezi, na kuwapeleka vijana kwenye kambi na safari za uvuvi, Bw Saunders kwa muda mrefu amekuwa mtu mashuhuri katika jumuiya ya eneo hilo.
Kwa miaka mingi, amekuwa akikabiliwa na uchunguzi mara mbili kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono yaliyotolewa na wanaume kadhaa wa asili kutoka jamii za eneo lake.
Shutuma hizo zilipeperushwa kwa mara ya kwanza mnamo 2020, lakini uchunguzi wa awali wa polisi uliofuata ulifungwa bila kufunguliwa mashtaka.
Alijiondoa kwa hiari kama Askofu wa Broome mnamo 2020, lakini anabaki kuwa askofu mstaafu.
BBC

Post a Comment