Kocha Taifa Stars afungiwa na CAF,asimamishwa na TFF
Shirikisho la soka barani Afrika, CAF limemsimamisha kwa mechi nane, kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Adel Amouruche kutokana na kauli yake ya kwamba Morocco ina ushawishi ndani ya Shirikisho hilo.
Siku chache zilizopita, kocha huyo alinukuliwa akisema nchi ya Morocco ina ushawishi ndani ya CAF, kiasi kwamba ina uwezo wa kupanga muda wa timu yake kucheza pamoja na waamuzi inaowataka.
Katika taarifa yake, CAF imesema imechukua uamuzi huo baada ya Morocco kumlalamikia kocha huyo raia wa Algeria.
Kwa adhabu hiyo, Shirikisho la soka Tanzania, TFF, nalo limemsimamisha kuendelea na kazi yake kwa muda usiojulikana.
Na kwa sasa, timu hiyo iliyo nchini Ivory Coast kwa ajili ya michuano ya Afcon, itamaliza mechi zake ikiwa chini ya makocha wazawa, Hemed Morocco na Juma Mgunda.

Post a Comment