SERIKALI YAJA NA MUAROBAINI WA ENEO LA MTANANA KUJAA MAJI
Waziri wa Ujenzi,
Innocent Bashungwa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi
Aisha Amour kuwasimamia wataalamu kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS)
kuhakikisha hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu uboreshaji wa miundombinu ya
barabara katika eneo Mtanana katika barabara kuu ya Morogoro – Dodoma uwe
umekamilika na kupitika vipindi vyote vya mwaka.
Aidha, Bashungwa amesema kuwa tatizo la kukatika mawasiliano ya barabara
kutokana na mvua za Elnino zinazoendelea kunyesha katika eneo la Mtanana jijini
Dodoma litakuwa historia mara baada ya Serikali kupata suluhu katika eneo hilo.
Ameyasema hayo leo Tarehe 19 Januari 2024, jijini Dodoma mara baada ya
kukagua eneo hilo ambapo mnamo tarehe 9 Januari, 2024 alimuagiza Mtendaji Mkuu
wa TANROADS, Mohamed Besta kufanya tathmini ya eneo hilo ambalo lilijaa maji na
kusababisha barabara hiyo kufungwa majira ya asubuhi.
"Wananchi Kama mlivyosikia tathmini ilivyowasilishwa mbele yenu, tumekuja
na mkakati wa muda mfupi na muda mrefu, mwezi Desemba au Januari mwakani
tutakuja hapa Mtanana kufuatilia tena suala hili", amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo
inaendelea kufanya tathmini ambapo pamoja na muarobaini wa kuleta suluhu katika
eneo hilo pia kuona namna ya kuvuna maji ya mvua yanayotuama hapo.
Ametoa wito kwa watanzania kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira
ikiwa ni pamoja na kuacha kukata miti ovyo na kulima kwenye maeneo
yasiyoruhusiwa kwani kufanya hivyo kunasababisha mafuriko na kuweza kufunga
mawasiliano ya barabara na kupelekea kuharibika kwa mundombinu hiyo.
Kadhalika, Amemuelekeza Katibu Mkuu Amour kuhakikisha usanifu wa eneo hilo
unakamilika mapema ifikapo mwezi wa pili kama walivyopanga ili kazi za ujenzi
wa makalvati na madaraja katika eneo hilo kuanza mara moja.
Bashungwa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka
fedha za dharura Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu
ya barabara na madaraja ili fedha hizo kuweza kutumika endapo mawasiliano
katika miundombinu hiyo yanapoharibika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mipango ya Mindombinu kutoka TANROADS, Eng.
Iftar Mlavi, amesema kuwa tangu tatizo la kujaa maji katika eneo hilo kutokea
kaguzi mbalimbali zimefanyika ikiwemo kuwa na timu ya uangalizi inayohusisha
TANRAODS pamoja na jeshi la Polisi na kukutana na Wizara ya Kilimo ili kutafuta
uwezekana wa kuwa na bwawa kwa ajili ya kuzuia maji yanayotiririka pamoja
na kujengwa kwa makalvati makubwa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka amesema kuwa Wananchi wa
Mtanana wanataka kuona suluhisho la kudumu linapatikana katka eneo hilo kwani
shughuli za kuchumi zimekuwa zikisimama kutokana na kero ya kujaa maji
katika ene hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini, Wizara ya Ujenzi

Post a Comment